Home » » BIL 1/- KUANZISHA MIRADI ITAKAYOTOA AJIRA KWA VIJANA.

BIL 1/- KUANZISHA MIRADI ITAKAYOTOA AJIRA KWA VIJANA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango.

KILIO cha vijana waliohitimu vyuo mbalimbali vya elimu ya juu cha kukosa ajira, kutokana na uchache wa nafasi hizo, kimesikika baada ya Serikali kutenga Sh bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2016/17, zitakazotumika kuanzisha miradi endelevu ya kiuchumi itakayotoa ajira kwa kundi hilo.
Hayo yamo kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17, uliowasilishwa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango, kwenye mkutano wa wabunge wote wa Bunge la Tanzania.
Akizungumzia kipaumbele cha pili katika mpango huo, Waziri Mpango alisema kuwa ni kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu. Alisema, Serikali imeona umuhimu wa kuangalia nguvu kazi ya vijana na kuipa fursa kwa kuitengea fedha.
Alisema, katika programu ya kukuza ajira kwa vijana, inayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2014/15 hadi 2018/19, lengo ni kuongeza fursa za ajira kwa kuwawezesha wenye nia na uwezo wa kuanzisha miradi endelevu kiuchumi, wajiajiri wengine, hususan wahitimu kutoka vyuo nchini.
Kwa kutambua hilo, katika mwaka huu wa fedha, Sh bilioni moja zimetengwa kuwawezesha vijana wasomi, kwa kuwajengea uwezo na pia kuwapa mafunzo kwa kutumia maofisa wa Halmashauri na viongozi wa vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) ili wasaidie vijana kufungua vyama vyao vya kuweka na kukopa.
“Tukiwawezesha vijana tutakuwa tumesaidia eneo kubwa, wengi wa wahitimu kutoka vyuo mbalimbali hawana ajira na si rahisi Serikali kuajiri wote,” alisema Dk Mpango. Sensa ya Watu nchini ya Mwaka 2012 inaonesha kuwa, idadi ya watu imeongezeka mara tatu kutoka milioni 12.3 kwa mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012.
Sera ya Vijana Tanzania ya Mwaka 2007 inatambua vijana ni watu wote wenye umri wa miaka 15 hadi 35, ambapo kulingana na Sensa ya Mwaka 2012 vijana wote nchini ni asilimia 34.7 ya watu wote.
Ukosefu wa ajira nchini kwa vijana unatajwa kupungua kutoka asilimia 13.2 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 11.7 mwaka juzi na kwamba bado jitihada zaidi zinatakiwa ili nguvu kazi hiyo isipotee bali iwe na mradi wa kiuchumi wa kufanya kwa kujiajiri wenyewe.
CHANZO: HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa