Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMATI ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeeleza kuridhishwa
na utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaotekelezwa
mkoani Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza,
alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba kamati imefurahishwa na
utekelezaji wa mradi huo baada ya kukagua miundombinu ya mradi
unaosimamiwa na Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
Alisema barabara, vituo vikuu na vidogo vimejengwa kwa viwango
vilivyokusudiwa. Alisema hatua zilizobaki ni uwekaji mifumo ya nauli kwa
njia ya kadi, kufunga mitambo ya kuongoza mabasi na kujenga uzio kwenye
kila kituo kikubwa.
Alisema kukamilika kwa hatua za mwisho kutategemea uharaka wa
serikali katika kutoa fedha zinazohitajika kuruhusu mabasi kuanza
kufanya kazi. Rweikiza alisema kamati imeridhika kuwa mradi utakomboa
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa utaondoa msongamano wa magari,
utachochea ukuaji wa shughuli za uchumi na kwa hiyo kuboresha maisha ya
watu.
“Tumeona mabasi yaliyoletwa ni mazuri, yataweza kubeba watu 80 na
150, pia yana kamera kwa ajili ya kudhibiti uhalifu na ajali,” alisema
Rweikiza na kuongeza kwamba kamati imeshauri nauli ziwe nafuu watu wa
vipato tofauti waweze kunufaika na mradi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utawala na Serekali za Mitaa (Tamisemi),
Suleiman Jaffo, alipongeza kamati hiyo kwa kufanya ziara na kuzungumza
na watendaji wa wakala huo na kupata ufafanuzi wa utekelezaji wake.
“Kuna hatua ndogo ndogo zinafanyiwa kazi. Muda si mrefu wakazi wa Jiji
la Dar es Salaam wataanza kunufaika na maradi”, amesema Jaffo.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment