BUNGE limesimamisha utekelezaji wa miradi yote mipya ya Shirika la
Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mpaka hapo Kamati na Wizara
itakapopitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG),
sambamba na kuitisha taarifa za utekelezaji wa miradi yote iliyofanywa
na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Aidha, imeagiza ukaguzi wa kina wa ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za
Makamu wa Rais kwa kuangalia usalama wa jengo, hesabu zilizotumika kama
zinaendana na thamani ya jengo na kama washauri walitoa ushauri wao
ipasavyo.
Akizungumza katika kuhitimisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya
serikali iliyofanywa na Kamati ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema NSSF ilitoa taarifa ya utekelezaji wa
miradi ikiwa haijitoshelezi kwa kutoonesha gharama zilizotumika mpaka
sasa, bajeti iliyopangwa kutumiwa na kiasi kilichosalia ili kubaini kama
fedha zilizotumika zinalingana na thamani ya ujenzi wenyewe.
Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa takribani siku tano kuanzia
Machi 29, mwaka huu, ilitembelea Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu na
Mahakama.
Akizungumzia taarifa za utekelezaji wa miradi iliyofanywa na mifuko
yote ya hifadhi za jamii, Mchegerwa alisema kamati yake inataka kupitia
taarifa zote za utekelezaji wa miradi sambamba na kupitia sera ya
uwekezaji ili kuangalia kama yamefuata taratibu na hakuna upotoshaji.
“Kwanza kuna madeni makubwa ambayo mifuko hiyo inadai kwa wapangaji
wao. Pia tunaangalia sera ya uwekezaji ili kujiridhisha kama ushauri wa
kitaalamu uliotolewa unakidhi matakwa ya ujenzi unaoendelea.
Aliongeza: “Kuna majengo mengi yamejengwa hayana wapangaji lakini
sera ya uwekezaji itatusaidia kujua kama inafuatwa. Pia itatusaidia
kubaini mapungufu yaliyojiri, maana wajumbe wengi wana wasiwasi kuwa
huenda ujenzi wa majengo unalenga kwa wahusika kupata asilimia 10 bila
kuangalia mahitaji halisi, kwani majengo mengi yako wazi.”
CHANZO:HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment