SERIKALI imesema ipo tayari kuwasilisha bungeni baadhi ya mikataba
ambayo itaonekana ina ulazima wa kufika bungeni ili kujadiliwa na
wabunge kwa niaba ya wananchi kabla ya kupitishwa.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema) aliyetaka
kufahamu ni kwa nini serikali inapitisha mikataba bila kuiwasilisha
bungeni.
Katika swali lake, Majala alisema kinyume cha matakwa ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoagiza mikataba kufikishwa bungeni
ili kujadiliwa, serikali imekuwa ikipitisha mikataba hiyo bila kufanya
hivyo.
Alisema pamoja na madhara mbalimbali, yanayosababishwa na hatua hiyo,
pia nchi imekuwa inapata hasara kubwa kutokana na baadhi ya watendaji
kupitisha mikataba hiyo kwa kushawishika na rushwa, hatua aliyosema
imechangia kushamiri kwa vitendo vya ufisadi nchini.
Waziri Mkuu akijibu swali hilo, alikiri kuwa ni kweli Bunge lina
wajibu wa kuisimamia serikali lakini yapo maeneo ambayo limetoa mamlaka
ya kisheria kwa serikali kutekeleza majukumu mbalimbali ili kuharakisha
maendeleo.
Alisema moja ya eneo ambalo wabunge kupitia Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wametoa mamlaka kwa serikali kutekeleza majukumu
yake ni katika eneo la mikataba, kwa Katiba kutoa nguvu ya kisheria kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kupitisha mikataba hiyo.
“Mwanasheria Mkuu anafanya kazi hii ya kupitia mikataba kwa niaba ya
serikali na Bunge, kama mikataba yote ingekuwa inakuja hapa bungeni ili
kujadiliwa na wabunge basi Bunge lisingekuwa na kazi nyingine zaidi ya
kupitia mikataba,” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.
Alisema hata hivyo hakuna ubaya, endapo wabunge watapendekeza
kuwasilisha bungeni mikataba ya kiwango au aina fulani ili ijadiliwe na
wabunge kwa niaba ya wananchi ili kulinda maslahi mapana ya taifa.
Kuhusu ufisadi katika mikataba, Waziri Mkuu alisema pamoja na
mikataba kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pale inapobainika
kuwepo kwa ukiukaji wa maadili na sheria za nchi, hatua mbalimbali
zimekuwa zinachukuliwa kwa wahusika wa suala hilo.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment