MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) ameitaka
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha
mahakamani wahusika wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow ili sheria
ichukue mkondo wake.
Zitto aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akichangia kwenye
hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora,
iliyowasilishwa na Waziri Angela Kairuki pamoja na ile ya Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyowasilishwa na
Waziri wake, George Simbachawene.
Alisema mwaka 2014, Takukuru waliijulisha Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi
kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kwenda Benki ya Stanbic Tanzania.
Alisema katika taarifa zote ambazo Takukuru inatoa kuhusu kesi za
ufisadi, hakuna mahali inapozungumzia maendeleo ya suala hilo. “Hata
siku moja hakuna mahala Takukuru wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini
wahusika waliochota fedha za umma watafikishwa mahakamani.
Naomba tupate kauli ya serikali kuhusu jambo hili kwani ni moja ya
jipu,” alisema Zitto ambaye aligusia suala la ukiukwaji wa Sheria ya
Bajeti. Alisema kuna ukiukwaji kadhaa wa sheria ya bajeti kama vile
sheria namba 11 ya mwaka 2015, ambapo kifungu cha 8 cha sheria hiyo
kinaeleza namna ambavyo mfumo wa Bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.
“Vifungu vya 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa
bajeti unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka mpango na miongozo ya
bajeti ipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Mwezi Februari kila
mwaka.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment