Home » » ‘Kikwete hakutumia Katiba kusamehe watuhumiwa EPA’

‘Kikwete hakutumia Katiba kusamehe watuhumiwa EPA’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete hakutumia ibara ya 45 ya Katiba kutoa msamaha kwa baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), wanaoelezwa kuamriwa kurejesha fedha walizochukua.
Aidha, alisema pale ambapo kuna makosa, Rais anaweza kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa au kupewa adhabu kwa kutumia ibara hiyo.
Alisema, “Mimi kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Rais mstaafu hakutumia kifungu hicho,” Dk Mwakyembe alisema bila kueleza kifungu kilichotumiwa.
Alisema hivyo jana bungeni mjini hapa, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyetaka kujua endapo Rais aliyepita alitumia madaraka yake vibaya, alikosea au alikuwa sahihi kuruhusu baadhi ya watuhumiwa walipe fedha walizodaiwa kuzifanyia ubadhirifu kupitia akaunti ya EPA (Hawakutajwa).
Pia, mbunge huyo katika swali lake la pili la nyongeza alitaka kujua ni lini watafikishwa mahakamani akieleza kuwa msamaha waliopewa haukuwa wa kikatiba na kwamba wanastahili kushitakiwa.
Katika swali lake la msingi, Haji alitaka kujua iwapo Rais ana mamlaka ya kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambayo mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi, upelelezi au mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 45 (1, A hadi D) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais ana mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo gerezani.
Akijibu, Dk Mwakyembe alisema, ibara hiyo inampa Rais mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama.
Mamlaka mengine ni kumwachilia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote. Pia ana mamlaka kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu pia anaruhusiwa kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu.
Alisema, kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba, msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na mahakama.
“Watuhumiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako katika hatua ya upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hii. Kwa sababu hiyo, Rais hawezi kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi, upelelezi au mahakamani,” alisema Dk Mwakyembe.
Aliongeza kuwa, hatma ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka husika za uchunguzi, mashitaka na mahakama.
Chanzo Gazeti La Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa