NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema polisi
wanaothibitika kuwabambikia watu kesi huchukuliwa hatua zinazostahili
ikiwemo kufukuzwa kazi, hivyo wananchi waelewe kwamba Serikali haifanyii
mzaha suala hilo.
Alisema na kutoa mfano wa askari watatu waliofukuzwa kazi hivi karibuni baada ya kuthibitika kumbambikia mtu kesi gerezani.
Alisema; “Ninaomba kuweka suala hili vizuri kwamba si askari wote
wanabambikia watu kesi na wala si jeshi lote la polisi linafanya hivyo.
Wanaohusika ni wachache katika matukio machache na wanapothibitika
huchukuliwa hatua stahiki.”
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini
(Chadema) aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani kukomesha tabia
ya askari wa Jeshi la Polisi kubambikia watu kesi.
Masauni alisema jamii inapaswa kuelewa kuwa Serikali haizembei
kuchukua hatua pindi inapohitajika kufanya hivyo kwa askari yoyote
anayebambikia mtu kesi.
Alikiri kuwa masuala hayo ya askari kubambikia watu kesi ni kweli yapo, ingawa alisema ni machache tofauti na inavyoelezwa.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment