Home » » NAPE: UANACHAMA WA TFF KATIKA FIFA UPO.

NAPE: UANACHAMA WA TFF KATIKA FIFA UPO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 
Na Benedict Liwenga-MAELEZO, Dodoma.

Kufuatia majadiliano na vikao mbalimbali vilivyofanyika mwaka 2005-2010, kumbukumbu zinaonyesha kuwa suala la uanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) lilifanyiwa kazi kwa ukamilifu na Serikali za pande zote mbili kwa ushirikiano na Vyama vyote viwili.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Mbunge wa Dimani Hafidh Ali Tahir lenye kipengele a,b na c lililotaka kujua ni nini matokeo ya Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu.

Mhe. Nnauye ameeleza kwamba, kwa kutambua umuhimu wa ZFA kupata uanchama wa FIFA, mwaka 2010 ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba, ukiongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri Kiongozi, Mhe. Juma Shamhuna pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Joel Bendera walikwenda Zurich, Switzerland ambako walikutana na Rais wa FIFA wa wakati huo.

Aidha, Mhe, Nnauye amefafanua kuwa, katika msafara huo walifuatana na viongpozi wa TFF na ZFA na madhumuni ya safari hiyo ilikuwa ni kuwasilisha maombi ya ZFA kupewa uanachama wa FIFA.

"Mwezi Juni 2011, FIFA iliiandikia ZFA ikiwajulisha kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, isingewezekana Zanzibar kupata Uanachama wa FIFA kwa kuwa wananchama wao ni nchi zinazotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyoelezwa katika aya ya 10 ya Katiba yao", alisema Mhe. Nnauye.

Mhe. Nnauye aliongeza kuwa, suala la usajili wa TFF au ZFA linafahamika vyema ndani ya Serikali ya Mapinduzi pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Hata hivyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa, uanachama wa TFF katika FIFA upo kwa mujibu wa muafaka wa pande zote mbili.

Kwa kuzingatia utaratibu wa FIFA kuhusiana na suala hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewaelekeza TFF nao wako tayari kufanya maridhiano na ZFA ili kukamilisha utaratibu wa wazi wa kukidhi mahitaji ya Zanzibar kushiriki katika masuala ya FIFA kupitia TFF bila kuathiri ushiriki wa klabu za Zanzibar katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa