Na Benedict Liwenga-MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI
imetenga Shilingi bilioni 59.5 katika Bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili
ya kuwawezesha Wananchi vijijini kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa kila
kijiji na mtaa.
Taarifa hiyo
imetolewa leo Bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Watu wenye
Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalum, Mhe. Esther Mahawe aliyetaka kujua ni lini fedha
zingetolewa na Serikali imejipanga vipi kutoa elimu ya ujasiriamali kwa
wananchi juu ya njia bora ya kutumia fedha hizo.
Dkt. Possi
amesema kuwa, fedha hizo zitatolewa mara baada ya kuidhinishwa na Bunge
hilo na baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga kuhakikisha
uwepo wa tija katika matumizi ya fedha hizo.
Ameongeza
kuwa, kuhusu mpango bora wa Elimu ya Ujasiriamali kwa wananchi, Serikali
inaendelea kukamilisha maandalizi ya utaratibu maalum wa utoaji wa
fedha hizo ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya Ujasiriamali.
"Baraza la
Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais,
TAMISEMI imepewa kazi ya kuratibu utekelezaji wa mpango huo", alisema
Dkt. Possi.
0 comments:
Post a Comment