KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeishauri serikali kuweka
utaratibu maalumu kwenye kanuni za sheria ya manunuzi kuruhusu baraza
jipya la madiwani kupewa taarifa ya mchakato wa manunuzi kwa kipindi
chote wakati baraza halikuwepo.
Ushauri huo unatokana na kamati hiyo kubaini kwamba kuna mapungufu
makubwa katika manunuzi ya umma hasa katika kipindi cha uchaguzi wakati
Kamati ya Fedha pamoja na Baraza la Madiwani huwa limevunjwa.
Akitoa taarifa kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa
Umma wa Mwaka 2016 uliowasilishwa juzi, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa
Ghasia alisema kwa sasa kanuni za uendeshaji wa halmashauri haziruhusu
Baraza la Madiwani kujadili taarifa ya manunuzi na taarifa nyingine
pindi baraza jipya la madiwani linapoingia.
Ghasia alisema kwa hali ilivyo inafaa kuwepo kwa kanuni inayotoa
ruksa kwa baraza jipya ili kuziba mianya ya manunuzi holela kipindi cha
Uchaguzi Mkuu.
Aidha, kamati hiyo imeitaka serikali wakati wa kuandaa kanuni
kuzingatia mazingira wezeshi yatakayosaidia wahisani wanaochangia miradi
ya maendeleo pale wanapohitaji serikali iwasaidie kugharamia baadhi ya
michango au huduma za haraka ambazo zitasaidia utekelezaji wa mradi
husika.
“Mfano wahisani wanaweza kutoa msaada wa vifaa vya hospitali kwa
masharti kwamba serikali itahitaji kuchangia bima na usafirishaji. Fursa
hizi zionenshwe kwenye kanuni hasa kwa upande wa miradi ya ubia (PPP)
itakayohusu ujenzi wa madarasa, barabara na miundombinu mingine katika
halmashauri na Serikali Kuu,” alifafanua Ghasia.
Pia kamati ilishauri serikali kuhakikisha kuwa taasisi za serikali
zinatoza bei ya soko ili zishindane katika soko na kupata wateja zaidi
kuliko sasa.
0 comments:
Post a Comment