Home » » Polisi yaonya wanaotaka kuvuruga mkutano wa CCM

Polisi yaonya wanaotaka kuvuruga mkutano wa CCM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
POLISI mkoani Dodoma imetoa onyo kwa watu watakaojaribu kuvuruga mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotarajiwa kufanyika Julai 23, mwaka huu .
Aidha, imeonya wakazi wa mjini hapa watakaobainika kuhifadhi watu wanaodhamiria kufanya vurugu kwenye mkutano huo kuwa pia watachukuliwa hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema watuhumiwa wanne waliokamatwa juzi ambao ni viongozi wa Baraza la Vijana (Bavicha) watafikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma zinazowakabili.
Watuhumiwa hao na vyeo vyao kwenye Bavicha ni Patrobas Katambi (Mwenyekiti- Taifa), Julius Mwita (Katibu Taifa) na George Tito ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo mkoa wa Mbeya.
Mwingine aliyekamatwa ni mratibu wa uenezi na uhamasishaji wa baraza hilo, Edward Simbeye. Wote walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha kashfa dhidi ya serikali.
Alitoa onyo hilo wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari na maofisa mbalimbali wa polisi wa mkoani juu ya kile alichoeleza, jaribio la kuleta vurugu katika mkutano huo wa CCM.
‘’ Jeshi halitawaacha bali hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale wenye nyumba binafsi ambao watawahifadhi wenye nia mbaya na mkutano wa CCM,’’alisema.
Alisema kumekuwa na viashiria vya kutokea vurugu katika mkutano huo na kusema polisi imejipanga kukabiliana na watakaohusika kusababisha hali hiyo.
“Tutahakikisha mkutano huo unakuwa ni wa amani na ole wako ulete vurugu katika mkutano huo, watafanya wale ambao utawahusu tu,’’alisema.
Kwa mujibu wa kamanda, wanaoshikiliwa walikamatwa wakiwa katika harakati za kuhamasisha wengine kuichukia serikali kwa kauli na mavazi yenye kubeba ujumbe wa uchochezi.
Mambosasa alisema kuwa polisi tayari wana taarifa kuwa watu hao wamepanga kufikia kwenye nyumba za watu binafsi badala za kulala kwenye nyumba za wageni, hivyo alidai wale wote watakaobainika kuwahifadhi watakamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na kosa la kuwatunza watuhumiwa hao.
Alisisitiza kuwa polisi haiko tayari kuona makundi hayo ya kisiasa yakivuruga amani na utulivu uliopo ndani ya mkoa huo wa Dodoma kwa kisingizio cha siasa na endapo yatajitokeza yatakutana na mkono wa sheria.
Chanzo Na Gazeti La Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa