Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Bunge
la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata msiba wa gafla wa
Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar Mhe. Hafidh Ali Tahir aliyefariki
leo majira ya saa 8 usiku kwa ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya
General iliyopo mkoani Dodoma.
Taarifa
hiyo imetangazwa leo Bungeni mjini Dodoma na Spika wa Bunge hilo, Mhe.
Job Ndugai na kusitisha shughuli za Bunge kwa ajili ya kupisha shughuli
za kuuaga mwili wa Mbunge huyo zilizofanyika katika viwanja vya Bunge
vilivyopo mjini humo kuanzia saa 3:30 asubuhi na kupelekwa uwanja wa
ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi
yatakayofanyika leo Novemba 11 mwaka huu.
Mhe,
Ndugai amesema kuwa marehemu Mhe. Hafidh Ali aliugua kwa muda mfupi
ambapo baada ya kujisikia vibaya aliamua mwenyewe kuelekea Hospitali
ndipo huko mauti yalipomkuta wakati akiendelea na matibabu Hospitalini
hapo.
“Ndugu
waheshimiwa wabunge kwa masikitiko makubwa naomba kuwatangazia msiba
tulioupata wa Mbunge mwenzetu Mhe. Hafidh Ali aliyefariki leo usiku
katika Hospitali ya mkoa wa Dodoma, kwa kweli tumeondokewa na Mbunge
mchapakazi, mwanamichezo, mcheshi na aliyewajali wapiga kura wake kwa
kiasi kikubwa”, alisema Mhe. Ndugai.
Akitoa
salamu za rambirambi kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa ametoa pole kwa wafiwa wote kwa kumpoteza mtu mahiri
aliyeshirikiana na wenzake katika shughuli mbalimbali za kitaifa pamoja
na kijamii.
“Ni
jambo la huzuni sana kwa Bunge letu na Serikali kwa ujumla kwa sababu
Mbunge mwenzetu alikua mchapakazi na alijitahidi kushiriki katika kamati
nyingi za Bunge hasa Kamati ya PAC, hii inaonyesha dhahiri kuwa
marehemu alikuwa ni mtu anaejali wenzake na wenzake wanathamini mchango
wake katika shughuli hizo”, alisema Waziri Mkuu.
Akitoa
salamu za rambirambi kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
Kiongozi wa kambi hiyo Mhe. Freeman Mbowe amesema kuwa Bunge limempoteza
Mbunge, Mwanamichezo pamoja na kiongozi hodari kwa kuwa katika kipindi
cha uhai wake alijitahidi kutoa mawazo chanya katika maamuzi mbalimbali
ya maendeleo pia aliishi vizuri bila kumbagua mtu kutokana na itikadi za
vyama.
“Mhe.
Hafidh Ali amemaliza safari yake hapa duniani hivyo kifo chake ni kama
somo kwa sisi tuliobaki, katika kipindi cha uhai wetu tutambue kuwa
tofauti zetu ni za muda mfupi hivyo natoa rai kwa wabunge wote kuungana
na kuwa kitu kimoja ili kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya nchi yetu
bila kujali itikadi ya vyama vyetu”, alisema Mhe. Mbowe.
Akiwakilisha
Timu ya mpira wa miguu ya Bunge (Bunge Sports Club), Mwenyekiti wa timu
hiyo, Mhe. William Ngeleja amesema kuwa marehemu alikuwa mwanamichezo
mahiri wa mpira wa miguu na muda mwingi wa maisha yake aliutumia katika
michezo.
“katika
enzi za uhai wake, marehemu aliwahi kuwa Mchezaji, Kocha na Mwamuzi wa
mpira kwa kiwango cha kimataifa wa timu yetu ya Bunge pia amewahi kupata
fursa za kuchezesha fainali za kombe za mataifa ya Afrika mara 9 pamoja
na fainali za kombe la Dunia kwa watoto chini wa miaka 17 hivyo
wanamichezo tumepata pigo kubwa sana”,alisema Mhe. Ngeleja.
Marehemu
Hafidh Ali Tahir alizaliwa Octoba 30 mwaka 1953 mjini Unguja, alimaliza
Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Bondeni, Unguja mwaka 1966
baadae mwaka 1985 alisoma masomo ya Habari na Utangazaji. Mnamo mwaka
1995 alianza shughuli za siasa ambapo mwaka 2005 alichaguliwa kuwa
Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar aliyeliongoza jimbo hilo hadi mauti
yalipomfika.
0 comments:
Post a Comment