Home » » MAMBO 10 KWA TAIFA YALIYOONGELEWA KATIKA KIKAO CHA TANO BUNGE LA 11.

MAMBO 10 KWA TAIFA YALIYOONGELEWA KATIKA KIKAO CHA TANO BUNGE LA 11.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ulikaa kwa muda wa siku 11 tangu Novemba 01 na kuhitimishwa Novemba 11 mwaka huu umewapa fursa wabunge kujadili na kutoa maamuzi katika mambo muhimu kwa Taifa.

Awali kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai alisema kuanza kwa mkutano huo kunafuatia kukamilika kwa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vilivyofanyika kwa muda wa wiki mbili mjini Dodoma ambapo kamati hizo zilikutana na kujadili  na kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Hali ya Bunge ni shwari na salama, nawasihi wabunge ambao bado hawajawasili Dodoma waje ili tuweze kuifanya kazi ya kuishauri Serikali”, alisema Mhe. Ndugai.

Hakika ukitaka kujenga nyumba imara ni vema ukaanza na kujenga msingi imara wenye kukidhi mahitaji ya nyumba inayojengwa.

Ili taifa liendelee kuimarika kiuchumi, kijamii na kisiasa, Bunge likiwa muhimili muhimu wa kuishauri na kuisimamia Serikali limetekeleza wajibu wake wa Kikatiba ipasavyo. Mambo 10 yaliyotekelezwa kwa manufaa ya taifa:

Bunge lilijadili, kupokea na kutoa maoni ambayo ndio dira na muongozo wa kuandaa Bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Serikali imeanza kuandaa bajeti hiyo kwa kufuata mwongozo uliojadiliwa kwa manufaa ya maendeleo ya nchi kwa mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango aliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 ambapo sekta ya viwanda ndio kipaumbele cha kwanza ambacho malighafi yake nyingi inapatikana nchini hususani kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili nyingine.

Waziri Mpango amesema maeneo yanayosaidia katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa ni pamoja na utalii, misitu na wanyamapori, madini, hali ya hewa, ushirikiano wa kikanda na kimataifa na utawala bora.

Vipaumbele vingine vinavyopendekezwa katika mpango huo ni kuweka msisitizo mkubwa katika kufungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha usalama wa chakula, afya, kuimarisha elimu, usimamizi wa maji safi na majitaka, nishati ya uhakika, upatikanaji wa ajira, hifadhi ya jamii, usawa wa jinsia na watu wenye ulemavu.

Bunge limejadili na kupitisha Miswada miwili ukiwemo Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016. Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupitishwa kwa Muswada huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kutoa maoni ambayo yamepelekea kuhitimisha kwa kuupitisha Muswada huo.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha tunatimiza malengo ya takribani miaka 20 iliyopita ya kuifanya taaluma hii ya habari kuheshimika kama zilivyo taaluma nyingine,” alisema Waziri Nape.

Waziri Nape ameongeza kuwa kwa sasa Muswada huo umeshapitishwa na kukiri kazi iliyobaki ni kutunga Kanuni ambapo amewaomba wadau wa tasnia ya habari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maoni yatakayopelekea kuwa na kanuni zenye tija kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju amesema kuwa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ni mwanzo mpya wa tasnia ya habari nchini ambapo amewaasa wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari kutambua kuwa haki mara zote huendana na wajibu, hivyo hakuna haki isiyo na wajibu.

Bunge lilitimiza wajibu wake wa kutunga Sheria kwa kupitisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ambao tayari Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameuridhia na amesaini Novemba16 mwaka huu ambapo sasa ni miongoni mwa Sheria kamili ya nchi.

Muswada mwingine uliojadiliwa wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016 uliowasilishwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju ukipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria 9 tofauti kwa lengo la kurahisisha utekelezaji madhubuti wa Sheria hizo hivyo, kuondoa upungufu unaojitokeza wakati wa kutumia Sheria hizo na pia kuoanisha masharti ya Sheria zinazorekebishwa na masharti yaliyopo katika Sheria nyingine zilizopo.

“Baadhi ya masuala yaliyozingatiwa katika Muswada huu ni kubadilisha vifungu vya Sheria kwa kufuta baadhi ya vifungu vya Sheria hizo na kuviandika upya, kufuta baadhi ya maneno kwenye vifungu vya Sheria, kuingiza maneno mapya na kuongeza vifungu vipya,”alisema Masaju.

Wabunge walipewa semina kabla ya kujadili Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU) (EPA) ili wapate uelewa na hatimaye kuishauri Serikali juu ya suala hilo.

Watoa semina hiyo walikuwa ni wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Saalam wakiongozwa na Prof. Palamagamba Kabudi, Dkt. Ng’waza Kamata na Dkt. John Jingu pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda.

Baada ya Semina hiyo, Bunge lilichukua jukumu lake la kuchambua na kujadili kwa kina Mkataba huo ambapo hatimaye Bunge limeafiki kuishauri Serikali kutosaini mkataba huo kwa kuwa umeonekana utazorotesha ukuaji wa uchumi wa nchi hasa kipindi hiki ambacho Tanzania imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda.

Akitoa maoni yake wakati wa mjadala Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema kuwa tatizo lililopo katika mkataba huo ni kutoitambua nchi kama nchi na badala yake kuangalia nchi zote kwa pamoja hivyo amewashauri wabunge kujadili kwa makini bila kuingiza itikadi za kichama.

“Kwa kuwa kifungu cha 143 cha mkataba huo kinaruhusu kupeleka marekebisho, naishauri Serikali yetu ipeleke marekebisho ya kupendekeza kila nchi iingie mkataba kivyake kulingana na maslahi ya nchi yake”, alisema Bashe.

Naye, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali amesema kuwa mkataba huo haufai kwa maslahi mapana ya Taifa kwani unataka kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini wakati nchi ya Tanzania inaingiza bidhaa nyingi kutoka nje kuliko kutoa bidhaa za ndani.

“Kama tukikubali tukaondoa ushuru wa kuingiza bidhaa kutoka nje basi tutapoteza mapato mengi yanayotokana na kuwepo kwa bandari pia tunatakiwa tujiulize kama mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru je nchi yetu ina bidhaa zinazokidhi vigezo vya kuingia katika nchi za Ulaya?” , alihoji Bobali.

Bunge limepokea Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na za Mitaa.

Aidha, kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Bunge limepata fursa ya kujadili taarifa ya Hesabu za Serikali ambayo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka ambapo Kamati iliishauri Serikali kuanzisha mfumo maalum wa uwekezaji ambao utatunza fedha zitakazowekwa katika mfuko huo na baadae kutumika kama mitaji katika maeneo ambayo nchi inataka kuwekeza.

“Sisi kama kamati tunaishauri Serikali kuanzisha mfuko maalum wa uwekezaji kwani utaisaidia Serikali kupata fedha za kufanyia maendeleo na kupata mitaji ya kuwekeza sehemu mbalimbali ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa na watanzania wanaiona faida ya uwekezaji,” alisema Kaboyoka.   

Mhe. Kaboyoka amefafanua kuwa Kamati imetoa ushauri huo baada ya kukwama kwa baadhi ya miradi pamoja na shughuli nyingine za Serikali zinazofanywa ili kuwasaidia wananchi kutokana na ukosefu wa fedha za kufanyia shughuli hizo hivyo kuanzishwa kwa mfuko huo kutahakikisha faida ya uwekezaji inaonekana.

Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) iliyowasilishwa Bungeni hapo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vedasto Ngombale Mwiru amezikumbusha Halmashauri hizo kutenga asilimia 10 ya fedha za mapato kutoka katika vyanzo vya ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana.

“Sisi kama Kamati tunaishauri Serikali kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya wanawake na vijana ili iwe sheria ambayo itatekelezwa kwa lazima hivyo kuendelea kuinua maisha ya wanawake na vijana kama ilivyokusudiwa,” alisema Ngombale Mwiru.

Pia kamati hiyo imetoa rai kwa Halmashauri zote nchini kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake kusimamia miradi mbalimbali kwa ukaribu ili iweze kukamilika kwa wakati na kutumika kama ilivyo kusudiwa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alitoa kauli ya Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017.

Prof. Ndalichako amesema kuwa jumla ya wanafunzi 119,012 wa Elimu ya Juu nchini wametengewa kiasi cha shilingi bilioni 483 katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kupewa mikopo itakayowasaidia kujikimu wakati wakiwa vyuoni.

Ameongeza kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa kuzingatia malengo ya Mfuko wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo kigezo kikuu kimekuwa ni uhitaji wa mwanafunzi pamoja na fani za kipaumbele anayosoma mwanafunzi.

“Kwa mujibu wa Wizara yetu, fani za kipaumbele ni pamoja na Sayansi za Tiba na Afya, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mifugo, Uhandisi wa Viwanda pamoja na Kilimo na Umwagiliaji lakini kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamedahiliwa kwenye fani za kipaumbele lakini hawana vigezo vya kupewa mikopo kutokana na tathmini ya uhitaji kuonesha kuwa wanaweza kusomeshwa na wazazi au walezi wao,”alisema Prof. Ndalichako.

Aidha, Prof. Ndalichako amesisitiza kuwa jumla ya wanafunzi 25,717 wanaoendelea na masomo waliokuwa na mikopo wataendelea kupatiwa mikopo hiyo kama ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita ambapo hadi sasa, wanafunzi ambao vyuo vyao tayari vimewasilisha taarifa za matokeo ya wanafunzi wao Bodi imekwishawatumia fedha zao za mkopo.

Katika taarifa hiyo, Prof, Ndalichako ameelezea kuwa taratibu za kuwabaini wanafunzi wasio na sifa stahiki zinaendelea na zitakapokamilika wanafunzi hao hawatopewa mkopo, ameahidi kufanya mapitio ya udahili wa wanafunzi vyuoni pamoja na utaratibu mzima wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo kwa lengo la kuwa na mfumo bora zaidi.

Kulingana na ratiba ya shughuli za Bunge, upo muda wa maswali ya Wabunge kwa Serikali ambayo hupatiwa majibu kutoka Wizara mbalimbali na taasisi zake. Pia kila siku ya Alhamisi wakati wa mikutano ya Bunge utaratibu wa wabunge kumuuliza Waziri Mkuu maswali ya papo kwa papo yasiyozidi 10 ambayo hujatolea majibu ya Serikali.

Aidha, wakati shughuli za Bunge zikiendelea, kumetokea misiba mitatu iliyohusisha Bunge ya kifo cha ghafla cha Mbunge mmoja aliyekuwa madarakani Hafidh Tahir Ali, Spika Mstaafu Samuel Sitta na Joseph Mungai. Vifo hivyo vimekuwa pigo kwa familia, Bunge na taifa kwa ujumla ambapo Wabunge walipata fursa ya kuwaaga waliotangulia mbele ya haki.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliahirisha Bunge hadi Januari 31 mwaka 2017 bila kusoma hotuba aliyoiandaa kutokana na misiba ya viongozi hao hatua iliyotoa fursa kwa Wabunge kushiriki mazishi kwenye maeneo husika walipozikwa viongozi hao. 
                    
Mwisho

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa