Benny Mwaipaja,
WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dokta Philip Mpango, amewataka wataalamu wa Mipango na Maendeleo
Vijijini kufanyakazi zao kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na
ufisadi ili kuwawezesha wananchi hususan waishio vijijini kunufaika na huduma
yao ili kujikwamua kiuchumi na kuodokana na umasikini
Dokta Mpango
ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini kilichoko eneo la MIYUJI mkoani Dodoma, ambapo wahitimu 1,641 wakiwemo
wanaume 796 na wanawake 845 wametunukiwa tuzo zao katika kozi 11 zinazohusu
Mipango, Maendeleo, Fedha na uwekezaji.
Amesema kuwa
ubunifu na upangaji mzuri wa mipango ya maendeleo vijijini utaharakisha nia ya
serikali ya kuwaondolea wananchi wake umasikini hivyo kuboresha maisha yao
Waziri huyo wa
Fedha na Mipango, amewahimiza wahitimu hao kuja na mawazo mapya au njia mbadala
za kukabiliana na changamoto za kukuza
shughuli za biashara vijijini, hasa ukosefu wa mikopo na mitaji, bima, mfumo
dume pamoja na mfumo duni wa uzalishaji na ukosefu wa masoko.
“Ninawaasa
wahitimu wetu muwe wazalendo na mfanyekazi kwa bidii kokote mtakako kwenda ili
muwe kioo cha chuo hiki kwasababu Tanzania yetu inawataka muwe wabunifu na
kukataa kujihusisha na mambo yanayohatarisha amani, usalama na umoja wetu kama
watanzania” aliongeza Dkt. Mpango
Aidha, amevishauri
vyombo vya habari nchini kuandika habari za changamoto na fursa zinazowakabili
wananchi vijijini badala ya kuandika na kutangaza mambo yanayodhalilisha nchi
yao kwa kukosekana uzalendo
“Tumeshuhudia mafanikio makubwa waliyoyapata
wakulima kutoka Wilayani Mbulu mkoani Manyara, na Njombe mkoani Iringa ambao
wameongeza uzalishaji wa mazao yao ya vitunguu saumu, mahindi na maharagwe pamoja
na kuongeza thamani ya mazao hayo, hizo ni habari nzuri za kuandika”
alisisitiza
Kwa Upande wake,
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, Dkt. Frank Hawassi, amesema
kuwa wahitimu wa chuo hicho wameandaliwa katika mfumo unaolenga weledi na
umahiri utakao wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa tija zaidi katika maeneo
yao ya kazi.
Amesema kuwa
wahitimu hao wameiva na wako tayari kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa
kimaendeleo katika kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Naye Mwenyekiti wa
Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Razack Lokina, ameiomba serikali
kukisaidia chuo hicho kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala,
hosteli na upungufu wa wahadhiri ili kukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa
elimu bora kwa wahitimu wake.
Akizungumza katika
mahafali hayo, Mwanafunzi bora wa shahada ya uzamili, Bi. Gemma Mafwolo,
amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameiva na wako tayari kutumika mahali
popote hapa nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi
vijijini.
“Tunapenda kukuahidi kuwa tutatumia elimu
tuliyoipata kwa manufaa mapana ya taifa letu kwa kuibua, kupanga, kutekeleza,
kusimamia, kufuatilia na kufanya tathimini ya mipango na maendeleo katika
nyanja zote za maendeleo” alisisitiza Mafwolo
Vilevile
ameishukuru serikali kwa kuahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo
hicho ikiwemo ukosefu wa sehemu za malazi ya wanafunzi, maeneo ya michezo
pamoja na upungufu wa wahadhiri.
Zaidi ya wataalamu
wa mipango ya maendeleo vijijini 14,583, wamehitimu mafunzo yao tangu chuo
hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kianzishwe mwaka 1980 kikisimamiwa na
Wizara ya Fedha na Mkipango.
Katika tukio
jingine, waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amezindua jengo la pili
la taaluma la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini lililojengwa kwa gharama
ya shilingi Bilioni 10.3 lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,250
wanaofundishwa kwa wakati mmoja.
Jingo hilo la
ghorofa 7 lina kumbi 4 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua watu 320 kila
mmoja, madarasa 6 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila moja, chumba
kimoja cha maabara ya kompyuta chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kwa
wakati mmoja, ukumbi 1 wa mikuta (80), Stoo 2, kantini 1 na vyumba vya ofisi
32.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment