Na: Lilian Lundo – MAELEZO - Dodoma
Bunge
la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha
muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka
2016 [The written laws miscellaneous Amendments (No. 4) Bill, 2016].
Akiwasilishwa
muswada huo Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema
kuwa muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Sita
ambapo lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kurahisisha utekelezaji
wa Sheria hizo kwa kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia
masharti ya sheria hizo.
Masaju
alizitaja sheria zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia muswada
huo kuwa ni Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sheria ya Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Sukari na Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori.
“Ibara
ya 21 ya muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 30 cha
Sheria ambacho kinaweka masharti kuhusu Waziri mwenye dhamana ya fedha
kukasimu madaraka yake chini ya Sheria hiyo. Sheria ilivyo sasa
inaelekeza kuwa Waziri anaweza kukasimu mamlaka yake ya kujadili mkopo
(negotiating loan), kuingia makubaliano ya kukopa mkopo na kutoa
dhamana,” alifafanua Masaju.
Aliendelea
kwa kusema kuwa muswada unapendekeza kuwa Waziri awe na uwezo wa
kukasimu pia mamlaka ya kujadili au kuingia makubaliano ya misaada kwa
mamlaka au mtu mwingine. Lengo la marekebisho hayo ni kurahisisha
taratibu za upokeaji misaada kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu
suala hilo.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba na
Sheria, Mohamed Mchengerwa alipokuwa akitoa maoni na ushauri wa kamati
hiyo alisema kuwa, kamati hiyo inaunga mkono marekebisho ya Sheria ya
Mkopo wa Elimu ya Juu kwa sababu itatoa nafasi kwa Watanzania wengi wa
kipato cha chini kupata nafasi ya kusoma katika Vyuo vya Elimu ya Juu.
Aidha
ameeleza kuwa, kamati inakubaliana na mtazamo wa Serikali kwamba utoaji
wa Mikopo ya Elimu ya Juu kwa ajili ya ngazi ya Diploma utazingatia
vipaumbele vya Taifa kulingana na wakati husika.
Nae, Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa amesema
kuwa muswada huo umelenga kusaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata mikopo yenye riba
nafuu.
Vile
vile muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria ya Wanyamapori
kuwa, katika hatua yoyote ya kesi ya Mahakama inaweza kwa kuamua yenyewe
au kwa maombi ya upande wa mashtaka kutoa amri kuwa
mnyama, nyara ya Serikali, silaha, gari au kitu chochote kilichotolewa
kama ushahidi ambacho kinaweza kuharibika au kupoteza thamani kiuzwe au
kiharibiwe na Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia
muswada huo unapendekeza kuongezwa kifungu kipya kitakachoweka masharti
kuhusu bei elekezi ya miwa, sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na
miwa.
Mwenyekiti,
Mhe. Najma Giga alitangaza rasmi kupitishwa kwa muswada huo na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi za ndio.
Aidha muswada huo unasubiri kibali cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ili uanze kutumika kama sheria.
Mwisho….
0 comments:
Post a Comment