SERIKALI YAFAFANUA MIKOPO KWA VIJANA, MALIPO ADA KWA FEDHA ZA KIGENI
Dodoma, Jumatano, 1 Februari, 2017:
Serikali imetoa
ufafanzi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vijana na
malipo ya ada kwa fedha za kigeni. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo
wakati wa kikao cha pili katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Kuwainua Vijana Kiuchumi
Akijibu hoja
kuhusu namna vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wanavyoweza kufaidika
kiuchumi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony
Mavunde, amesema Serikali imetenga fedha za kutosha kupitia mifuko mbalimbali
kuwawezesha vijana kwa mitaji na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwainua kiuchumi.
Ameongeza kuwa
vijana wenyewe ndio wanaopaswa kuchangamkia fursa hizo na pale wanapojiunga katika
vikundi mbalimbali wamekuwa wakipewa mikopo kwa ajili ya mitaji. Alitoa mfano
wa jinsi Serikali ilivyowawezesha vijana waliojiunga na kuwekeza katika viwanda
vidogo vya maziwa na chaki mkoani Simiyu.
Amewataka pia
Wabunge na Halmashauri zote nchini kuendelea kupigania kutengwa maeneo maalum
katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia vijana na kutengwa kwa asilimia
5 ya mapato ya Halmashauri kwa maendeleo ya vijana
Ada
kwa Fedha za Kigeni
Serikali
imesema, ingawa haijapokea malalamiko yoyote kuhusu wananchi wasioridhihwa na mtindo
wa kutakiwa kulipa malipo ya ada kwa fedha za kigeni katika baadhi ya shule na
vyuo, lakini imesisitiza kuwa wale wanaotoza ada kwa fedha za kigeni wanakiuka
Sheria.
Akitoa
ufafanuzi huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella
Manyanya amesema kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania
(BOT), 2006, fedha inayopaswa kutumika kwa malipo ya huduma nchini ni Shilingi
ya Tanzania. Ameviagiza vyuo na shule nchini kuacha kutoza ada kwa fedha za
kigeni na kuhimiza wananchi watakaobainika kufanya hivyo kutoa taarifa
Serikalini.
Si Tatizo Kutumia Majengo UDOM
Serikali imesisitiza
kuwa baadhi ya Wizara zilizoanza kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma kutumia
baadhi ya majengo kwa muda kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakutaathiri
shughuli za chuo.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. Waziri Jenista amesisitiza kuwa baadhi ya
Wizara zitatumia majengo ya UDOM kwa sababu mengi ya majengo hayo yalikuwa
hayatumiki kwa sasa kwa shughuli za chuo hicho na hakutakuwa na muingiliano na
shughuli za chuo.
Mradi wa Mabilioni Maji Dar
Serikali kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Maji Dar es Salaam imeanza kutekeleza mradi wa
usambazaji wa maji utakaogharimu Dola za Marekani milioni 32.772 ambazo ni
mkopo kutoka Benki ya Exim ya China. Mradi huo utahusisha sehemu yote ya jimbo
la Kawe, Dar es Salaam. Mradi huo utachukua miezi 15.
Imetolewa na:
Idara-Habari Maelezo
Idara-Habari Maelezo
0 comments:
Post a Comment