Na. Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali
itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous
kutokana na ukiukwaji wa taratibu zilizokuwa zimewekwa wa kuingia ndani
ya hifadhi hiyo.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani ameyasema hayo leo
Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji
Mohamed Mchengerwa juu ya hatua ambazo Serikali inazichukua kutoa ridhaa
kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria kuweza
kuvua samaki.
“Mwaka
1994, wananchi wa Kata ya Mwaseni, Mloka, Ngoroka na Kipungila Wilaya
ya Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua
Samaki. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa
zimewekwa kwa kuingia ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua
samaki kinyume cha sheria,” alifafanua Mhandisi Makani.
Aliendelea
kwa kusema kuwa baadhi ya wavuvi walibainika kujihusisha na vitendo vya
ujangili wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti
ovyo kwa ajili ya kukausha samaki na kutengeneza mitumbwi pamoja na
uharibifu wa mazingira uliotokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha
sheria.
Mhandisi
Makani amesema kuwa kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya
uhifadhi wa wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea
kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous.
Aidha
Wizara inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo
zilizo jirani kutumia mabwawa mengine yaliyoko nje ya Pori hilo yenye
fursa kubwa kwa kufanya shughuli za uvuvi.
Mabwawa
ambayo wananchi wameshauriwa kuyatumia ni Bwawa la Zumbi lililoko
vijiji vya Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe lililopo Mkongo,
Lugongo lililopo kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini lililopo Mji wa
Kibiti.
Mabwawa hayo ya Mto Rufiji yatatoa fursa ya shughuli za uvuvi hivyo kusaidia kuinua kipato cha wananchi.
Vile
vile Mhandisi Makani amesema kuwa, Wizara hiyo kwa kutambua mahitaji ya
wananchi katika maeneo hayo ya kufanyia kazi na kujiletea maendeleo
kiuchumi na kijamii. Wizara hiyo inaendelea kushauriana na Halmashauri
ya Wilaya ya Rufiji kuhusu namna ya kutekeleza mpango wa kuwajengea
mabwawa ya samaki ili pamoja na mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe
kufanya shughuli za uvuvi endelevu.
Mwisho..
0 comments:
Post a Comment