Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kwamba
vita inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na
matumizi ya dawa ya kulevya ni kubwa na kila Mtanzania anapaswa kuunga
mkono jitihada hizo.
Kassim
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Bungeni, Mjini Dodoma katika hotuba yake
ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
“Moja
ya eneo lililojadiliwa na kuibua hisia kali ni kuhusu vita inayoendelea
nchini dhidi ya dawa za kulevya. Watanzania wote ni mashahidi kwamba
vijana wetu wengi wameendelea kudhoofisha afya zao kutokana na matumizi
ya madawa ya kulevya. Dawa za kulevya ni hatari kwa usalama na ustawi wa
Taifa,” alifafanua Waziri Mkuu.
Aliendelea
kwa kusema kuwa kitaalamu madhara ya kiafya yanayosababishwa na
matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu
kwa mtumiaji ikiwemo kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi usioponyeka kirahisi
na kusababisha vifo ikiwa mtumiaji atazidisha matumizi ya dawa hizo.
Aidha
Waziri Mkuu amesema kuwa madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na
magonjwa hayo ni pamoja na kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya,
gharama kubwa za uchunguzi wa kimaabara kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia
na kuendesha maisha yao.
Amesema
kuwa madawa hayo huingia nchini kwa kutumia bandari bubu kupitia Bahari
ya Hindi na kwa njia ya magari binafsi kupitia mipaka ya nchi ya Kenya,
Uganda na mpaka wa Tunduma.
Kassim
Majaliwa amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na
dawa hizo na kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya
wauzaji na wasambazaji.
Amewashukuru
wabunge kwa kutoa mchango mkubwa na ushauri wa namna nzuri zaidi ya
kupambana na janga hilo ikiwa dhamira ya Serikali ni kupambana na janga
hilo kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya
sheria na haki.
Kassim
Majaliwa ametoa takwimu ya Watanzania ambao wamefungwa katika magereza
mbalimbali nje ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Watanzania 200 ambao
wamefungwa China, Watanzania 12 nchini brazil, Watanzania 63 nchini
Iran, Watanzania 7 nchini Ethiopia na Watanzania 296 ambao wamefungwa
Afrika ya Kusini.
Mwisho…
0 comments:
Post a Comment