Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote za Umma ambazo zinadaiwa
na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuhakikisha zinalipa madeni yao kabla
ya Juni 30, 2017.
Waziri
Mkuu ametoa rai hiyo leo, Mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge wakati
wa uzinduzi wa huduma ya 4G LTE za kampuni hiyo ya simu kwa Mkoa wa
Dodoma.
“Kuhusu
shilingi Bil. 11.5 ambazo TTCL inazidai Taasisi mbalimbali za Umma,
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, kaa na wadaiwa sugu
wote, thibitisheni madeni husika kisha mkubaliane namna ya kulipa
madeni hayo. Nijuavyo kila Wizara inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za
simu, sasa hayo malimbikizo yanatoka wapi?” alisema Kassim Majaliwa.
Aidha
amezitaka Taasisi hizo zinazodaiwa na TTCL kuhakikisha zinakamilisha
madeni yao kabla ya kufikia Juni 30, 2017 ili kampuni hiyo iweze kufanya
kazi ipasavyo na kuendana na ushindani wa kibiashara uliopo.
Pia,
ameitaka kampuni hiyo kujifunza kutoka kwenye makampuni binafsi namna
yanavyoendeshwa na kuiga baadhi ya mbinu zao, hususan katika kupunguza
gharama za uendeshaji.
Kassim
Majaliwa amesema kwamba, Serikali ina matarajio makubwa kutoka katika
kampuni hiyo kutokana na kuwa na imani kwamba kampuni hiyo ina maarifa
ya kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa kwenye sekta hiyo.
Vile
vile ameitaka kampuni hiyo kujifunza kutoka katika mashirika ya Umma ya
Simu kwenye nchi nyingine ambayo yanajiendesha kwa faida, kwa kuiga
mbinu ambazo wanazitumia na kuziweka katika muktadha wa nchi ya
Tanzania.
Waziri
Mkuu amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa pamoja na timu yake kwa hatua ambayo kampuni hiyo imefikia.
Aidha amemtaka Waziri huyo kufuatilia kwa karibu kampuni hiyo ili iweze
kutoa ushindani wa kutosha kibiashara, ijiendeshe kwa faida, itoe gawiwo
stahiki kwa Serikali, ilipe kodi na zaidi ya yote fedha za Umma
zilizowekezwa ziweze kutumika vizuri.
Mwisho.....
0 comments:
Post a Comment