Na: Lilian Lundo – MAELEZO-Dodoma.
Waziri
wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema kuwa viwanda
vitajengwa na Sekta Binafsi, na kazi ya Serikali ni kutengeneza
mazingira mazuri ya kujenga Viwanda.
Mwijage
ameyasema hayo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa majibu kuhusu
ufinyu wa bajeti wa Wizara hiyo ikiwa itatosheleza kujenga Viwanda
nchini, wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mwijage
amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Serikali kufikia uchumi wa
Viwanda ni kutengeneza mazingira mazuri ya kujenga viwanda ikiwa ni
pamoja na kuwatafuta wawekezaji ambapo mpaka sasa Serikali imeshaongea
na wawekezaji toka China, Uturuki na Misri na wote wameonyesha nia ya
kujenga viwanda nchini.
Kwa
upande wake Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema kuwa ni jukumu
la kila kiongozi kushiriki katika ujenzi wa Viwanda kwa kutambua fursa
zilizopo eneo ambalo analisimamia.
“Sera
ya kuwa na Tanzania yenye Viwanda haitawezekana kwa kuiachia Wizara ya
Viwanda peke yake bali kwa sisi wabunge pia kushiriki kupitia fursa
ambazo zinatuzunguka,” alifafanua Ridhiwani.
Vilevile
amesema kuwa ni muhimu Serikali kuendelea kuboresha hali ya umeme kwani
Viwanda kwa asilimia kubwa vinaendeshwa kwa kutumia umeme wa kutosha na wa uhakika.
Nae,
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa fedha
zinazopelekwa Wizara ya Viwanda si kwa ajili ya kujenga viwanda bali kwa
ajili ya kuzielekeza sekta binafsi zilipo fursa za kujenga viwanda.
Aidha,
Mwijage amesema kwamba mpaka sasa jumla ya viwanda 2169 vimesajiliwa
ambapo viwanda 170 vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),
viwanda 180 vimesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni,
viwanda 1,843 vimesajiliwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo
(SIDO) na viwanda 7 vimesajiliwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC)
vikiwemo viwanda 3 vya madawa.
Mwisho…
0 comments:
Post a Comment