Dodoma, Ijumaa, 10 Februari, 2017:
Serikali imefafanua
masuala mbalimbali yaliyoulizwa na Wabunge ikiwemo masuala ya utozaji wa kodi
wa hoteli (Hotel levy), suala la
wanunuzi wa korosho kutolipwa kwa wakati, ahadi ya kuboresha maisha ya wavuvi na
wakulima, utekelezaji wa REA III.Ufafanuzi huo umetolewa leo Bungeni Mjini
hapa.
Kukusanya Kodi katika Hoteli za Kitalii
Serikali
imesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Hoteli, Halmashauri haziruhusiwi
kukusanya kodi katika hoteli za kitalii. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
Selemani Jafo ametoa kauli hiyo leo Bungeni akisema kuwa Halmashauri
zinaruhusiwa kwa mujibu wa kifungu cha 26(3) cha Sheria hiyo kukusanya ushuru
wa hoteli katika nyumba za kulala wageni zilizokoko ndani ya halmashauri.
Ameongeza
kuwa, halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za
Mitaa Sura 290 kifungu cha 6(u) kukusanya ushuru wa huduma (Service levy) katika hoteli za kitalii zinazoendesha shughuli zake
ndani ya halmashauri kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya
Taasisi husika.
Wanunuzi wa Korosho kutolipa Wakulima Kwa wakati
Serikali
imesema kuwa, kupitia Bodi ya Korosho imekuwa ikihimiza wanunuzi kufuata
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Mamlaka husika. Kauli hiyo imetolewa
na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Ole-Nasha.
Amesema
kwamba, Serikali kupitia Sheria ya Korosho Na.18 ya Mwaka 2009 Kifungu Na.17 na
Kanuni za mwaka 2010 Kanuni ya 33 itaifungia kampuni yoyote kufanya biashara ya
korosho nchini endapo itakiuka Sheria na Kanuni ikiwemo ya kutowalipa wakulima
kwa wakati ili kubaki na makampuni yanayotii Sheria.
Ahadi ya Kuboresha Maisha ya Wavuvi na Wakulima
Kuhusu suala
la kuboresha maisha ya wavuvi na wakulima, Naibu Waziri Ole-Nasha amefafanua
kuwa, Serikali imeendelea na jitihada zake za kuwajengea mazingira mazuri
wakulima na wavuvi nchini kwa kuhakikisha kuwa, gharama kubwa za pembejeo na
vyombo vya uvuvi zinapungua ili waweze kuzipata kwa bei nafuu kwa kutenga kiasi
cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ruzuku ya zana za uvuvi, na jumla ya
shilingi bilioni 26.99 kwa ajili ya ununuzi wa mazao katika bajeti ya Wizara ya
mwaka 2016/17.
Aidha, amesema
kuwa, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umetengewa shilingi bilioni 15.0 na
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko shilingi bilioni 8.95. Pia amefafanua
kuwa, Serikali haikopeshi wavuvi, bali inaweka mazingira wezeshi kwa wavuvi hao
kupata mikopo yenye riba nafuu ambapo, kupitia Benki ya Rasilimali (TIB)
imeweka Dirisha la Kilimo Kwanza kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na
wavuvi. Ameongeza kuwa, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB)
ambayo baadhi ya majukumu yake ni kuwapatia wakulima na wavuvi mikopo yenye
riba nafuu.
Utekelezaji wa Mradi wa REA III
Serikali
imesema kwamba, jumla ya Vijiji 37 ambavyo havijapatiwa umeme katika jimbo la
muheza na vitongoji 137 vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme wa
Vijijini (REA) Awamu ya Tatu. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard
Kalemani ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Usambazaji Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu (REA III) kwa nchi nzima unatarajiwa kufanyika kwa mgawanyo wa
vipengele vitatu vya Densification, Grid
Extension pamoja na Off-Grid
Renewable.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
0 comments:
Post a Comment