MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Mkoa wa
Dodoma, uhakikishe unaondoa vitendo vya ukiritimba kwa baadhi ya
watendaji wa serikali, ambavyo vinaweza kusababisha ucheleweshaji au
kukwamisha ujenzi wa miji mipya mikubwa mitano ya kisasa katika maeneo
mbalimbali ya mkoa huo.
Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akifanya mazungumzo na viongozi
wa Mkoa wa Dodoma baada ya kupokea taarifa ya Kikosi Kazi, kilichoundwa
na serikali kwa ajili ya kuratibu shughuli mbalimbali za serikali
kuhamia Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi
yake, Makamu wa Rais amesema ni muda muafaka sasa hivi kwa uongozi wa
mkoa kujiimarisha na kujipanga ipasavyo katika kupokea wawekezaji wenye
nia njema ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani humo hasa wakati
huu ambao serikali inahamia humo.
Ameonya kuwa wawekezaji matapeli kamwe wasipewe nafasi ya kuwekeza
Dodoma na ametaka uongozi wa mkoa kuwa makini makundi hayo ili wasije
kuvuruga mipango ya serikali ya kujenga Makao Makuu ya kisasa katika
Manispaa ya Dodoma.
Pia ameuagiza uongozi wa mkoa, kulinda na kuendeleza maeneo yote
yenye uoto wa asili ili yasije yakaharibiwa kutokana na uwekezaji
utakaofanyika mkoani humo.
Alisema amefurahishwa na kasi ya uongozi wa Mkoa wa Dodoma, jinsi
unavyojipanga katika kuhakikisha azma ya serikali ya kuhamia Dodoma
inafanikiwa kwa haraka ikiwemo utengaji wa maeneo kwa ajili ya uwekezaji
wa viwanda na huduma za kijamii.
Kuhusu maeneo ya wafanyabiashara ndogo, Makamu wa Rais amewataka
viongozi wa Mkoa wa Dodoma wahakikishe wanatenga haraka maeneo maalumu
kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ili nao wanufaike na mpango wa
serikali kuhamia mkoani humo.
“Ni muhimu maeneo yote yatakayotengwa kwa ajili wafanyabiashara ndogo
yawe huduma zote za msingi ili kusaidia wafanyabiashara hao waweze
kufanya kazi zao kwa ufanisi,” alisisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa ni muhimu kwa uongozi wa Mkoa wa
Dodoma, kuwashirikisha viongozi wa wafanyabiashara ndogo kuhusu maeneo
yatakayotengwa ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao
kupewa maeneo yasiyofaa wa ajili ya shughuli zao.
Awali, kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na viongozi wa
mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alimweleza Makamu wa
Rais mipango na mikakati ya mkoa huo kuhusu azma ya serikali ya kuhamia
Dodoma ikiwemo kuimarisha huduma za msingi ikiwemo afya, miundombinu,
maji na elimu.
Alisema mpaka sasa kazi ya kuainisha maeneo mbalimbali kwa ajili ya
uwekezaji, makazi na mahali ambapo ofisi za serikali na za mabalozi
zitajengwa umeshakamilika.
Alisema wataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali,
mashirika ya kimataifa na mabalozi ili kuhakikisha maeneo yaliyotengwa
yanaendelezwa haraka.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment