Mwanariadha Alphonce Simbu akiwa katika moja ya Mashindano ya Riadha Picha kwa Hisani ya Gazeti la The Citizen
Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, leo tarehe 27 Aprili limezizima kwa nderemo na
shangwe pale alipotambulishwa rasmi mwanariadha Alphonce Simbu, Mshindi
wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon, na moja ya washindi wa London
Marathon.
Mwanariadha huyo ambaye
pia ni balozi maalum wa DStv, alilitembelea Bunge kama mgeni maalum wa
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Harison Mwakyembe akiambatana na
muwakilishi wa DStv Johnson Mshana na maafisa kadhaa waandamizi wa Jeshi
la kujenga Taifa akiwemo Kanali K.J Mziray – Mkuu wa Utawala na Mafunzo
wa JKT
Mara baada ya naibu
spika wa Bunge Dk. Tulia Akson kumtaja Simbu, bunge lilizizima kwa
shangwe kwa muda hali iliyoashiria kuraha kubwa kwa wabunge kuweza
kumshuhudia mwanariadha huyo ambaye ni tegemeo kubwa la Tanzania katika
mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu
jijini London.
Baada ya ziara hiyo,
Simbu alipata fursa ya kusalimiana na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Kassim Majaliwa na kisha kuwa na mazungumzo mafupi na
Waziri Mwakyembe.
Akiongea wakati wa
kupiga picha ya pamoja na Simbu, Waziri mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza
sana mwanariadha huyo na kusema kuwa Serikali inatambua na kuthamini
sana jitihada zilizofanywa na wadau wote katika kufanikisha ushindi wa
Simbu. Pia alimtakia kila la heri katika maandalizi na kisha ushiriki
wake katika mashindano ya Dunia yanayomkabili mwishoni mwa mwaka huu.
Naye Waziri mwenye
dhamana ya Michezo Harison Mwakyembe ambaye ndiye aliyemualika Simbu
Bungeni, alisema kuwa wizara imekuwa ikishirikiana na wadau kwa karibu
ambapo hata wakati wa Safari ya Simbu kwenda London, wizara ilihakikisha
safari hiyo inafanikiwa. Ameonyesha kufurahishwa kwake na vipaji
vilivyopo na kusema nguvu za ziada zitawekwa ili kuhakikisha kuwa vipaji
hivyo vinaibuliwa na kukuzwa kwa manufaa ya taifa zima.
Kwa upande wake, Simbu
alisema kitendo cha yeye kualikwa bungeni kimempa faraja kubwa na pia
alifurahi sana kuona jinsi wabunge walivyomshangilia na kumpongeza.
“Kwakweli ujio wangu bungeni umenipa faraja kubwa kuona ni jinsi gani
wabunge wote walivyofurahishwa na mafanikio niliyopata na sifa
niliyoiletea nchi. Hii imenipa sana moyo na uzalendo kwani ni dhahiri
kuwa taifa zima liko nyuma yangu na linanunga mkono kikamilifu” alisema
Simbu
Alitoa shukrani za
pekee kwa wadhamini wake DStv, pamoja na Waziri Mwakyembe kwa jitihada
kubwa anazofanya. Amesema anaamini kwa mwenendo huu yeye, wanariadha
wengine na wanamichezo wote wa Tanzania watafika mbali na hatimaye
Tanzania itakuwa kinara katika ulingo wa michezo duniani. Pia
alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kumruhusu kufanya mazoezi na
kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Simbu ambaye ni
miongoni mwa wanariadha bora wa Tanzania alivunja rekodi yake aliyoiweka
mwaka jana nchini Japan ya muda wa 2:09:19 na hatimaye katika
mashindano ya London Marathon mwaka huu alitumia muda wa 2:09:10 ambao
ndio muda wake bora zaidi.
Simbu ni miongoni wa wachezaji wa timu ya taifa ya riadha watakaoshiriki mbio za Dunia mwezi Agosti mwaka huu jijini London.
0 comments:
Post a Comment