Na.
Immaculate Makilika, MAELEZO -DODOMA
Kila mtanzania ametakiwa kuhakikisha anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa miaka 53 iliyopita.
Akizungumza leo wakati
akihutubia wananchi katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano
katika uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa ni muhimu watanzania wakalinda
Muungano kwa vile una manufaa kwa nchi zote mbili.
“Kila mtanzania
ahakikishe anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wetu, kwa vile
Muungano na amani iliyopo nchini ndio
chachu ya maendeleo yetu” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli
alisisitiza kuwa “Muungano ndio silaha yetu, ni nguvu yetu, mimi na mwenzangu
Dkt. Shein tutaulinda Muungano kwa nguvu zote na yeyote atakayejaribu kuuvunja
atavunjika yeye” alisema Rais Magufuli
Akitaja baadhi
ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka 53 ya
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar
ni pamoja na kuunganisha mataifa
mawili na kuunda taifa moja lenye nguvu.
Rais Magufuli alitaja
mafanikio mengine ni pamoja na kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini, nchi
kavu na reli, kukabiliana na matatizo ya umaskini, ukosefu wa ajira na kukua kwa uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania
na mataifa mbalimbali ambapo yamepelekea mafanikio katika nyanja za kiuchumi,
kisiasa, na jamii.
Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa sherehe za Maadhimisho
ya Muungano kufanyika mkoani Dodoma ambapo, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali
imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kujenga miundombinu ili kufikia azma yake
ya kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma ifikapo mwaka 2020.
“Niwahakikishie wana
Dodoma na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na
hatutarudi nyuma tena,ambapo awamu ya kwanza ya watumishi wa Serikali takribani
3,000 kwa ngazi za Mawaziri,Naibu Waziri,Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu
wameshahamia Dodoma, kama tulivyoahidi kufikia mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia hapa”,
alisisitiza Rais Magufuli.
Sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano zenye
kauli mbiu isemayo “Miaka 53 ya Muungano, tuulinde na kuimarisha, tupige vita dawa za
kulevya na kufanyakazi kwa bidii”, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa serikali pamoja na wajane wa viongozi
waasisi wa Muungano ambapo ni Mama Maria
Nyerere na Mama Shadya Karume.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment