SERIKALI YAFAFANUA KUSHAMIRI KWA BIASHARA YA VYUMA CHAKAVU, MPANGO
WA KUUNDA BODI MPYA YA TUMBAKU NA UTENGAJI
ASILIMIA MAALUM KWA WANAFUNZI KUTOKA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR
Dodoma,Jumanne, 11 April,
2017.
Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu kushamiri kwa Biashara ya vyuma chakavu,Mpango wa kuunda bodi mpya ya Tumbaku na Utengaji
wa asilimia maalum kwa wanafunzi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Ufafanuzi huo umetolewa leo
Bungeni mjini Dodoma.
Kushamiri
kwa Biashara ya Vyuma Chakavu
Serikali imesema kuwa,
imekwishaandaa Rasimu ya Muswada wa Sheria itakayoweka bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na
udhibiti wa biashara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za
uzalishaji,ukusanyaji,usambazaji,uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia
uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.
Hatua hiyo imekuja baada ya
kuongezeka kwa mahitaji ya vyuma chakavu hapa nchini na duniani kwa ujumla na
kubainisha maeneo yaliyoathirika sana kuwa ni mifumo ya kusafirisha Umeme,Reli
na Barabara.
Akifafanua kuhusu
hoja hiyo, Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles
Mwijage amesema Muswada huo umeweka bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu
atakayebainika kuharibu miundombinu.
Aidha
Mhe.Mwijage ametoa wito kwa Wananchi wote kutoa taarifa pindi waonapo mtu
anayehujumu miundombinu kwa namna yoyote ile.
Mpango wa kuunda Bodi mpya ya Tumbaku.
Serikali imesema kuwa, iko
katika maandalizi ya kuunda Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Tumbaku haraka
iwezekanavyo na Wananchi watajulishwa kupitia tamko la Serikali mara baada ya
taratibu kukamilika.
Naibu Waziri wa
Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mhe.William Ole Nasha amesema kuwa, Serukali ilivunja
Bodi ya Tumbaku kwa lengo la kufanya maboresho katika utendaji kazi wake.
Ameongeza kuwa, hatua ya
kuvunja Bodi hiyo haihusiani na kusitisha shughuli zinazotekelezwa katika Kilimo
cha Tumbaku kwani wapo wataalamu wanaondeleza utekelezaji wa mpango uliopo wa
kuendeleza zao la Tumbaku nchini.
Aidha kwa kuzingatia kuwa
wakulima wanahitaji huduma muda wote hasa kipindi hiki cha kuelekea masoko ya
tumbaku kwa msimu wa 2017/18,Serikali kupitia mrajis wa vyama vya Ushirika nchini
imeshateua timu nyingine ambayo ipo Mkoani Tabora ikiendelea kuratibu na
kusimamia masuala mbalimbali ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuandaa upatikanaji
wa pembejeo kwa msimu ujao.
Serikali kuendelea kutenga fedha kwa wahitaji wa Mikopo ya Elimu
ya juu.
Serikali imesema kuwa
itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu kwa
kuzingatia Sheria,kanuni na taratibu na miongozo itolewayo mara kwa mara na
serikali kupitia bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu.
Naibu Waziri wa
Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhe. Stella Manyanya amesema kuwa utoaji wa
Mikopo unazingatia muombaji awe raia wa Tanzania,muhitaji,mlemavu au yatima na mabaye
amedahiliwa katika elimu ya juu na mwenye kuchukua programu za vipaumbele vya
Taifa kama Sayansi, Hisabati,uhandisi wa
Gesi na Mafuta, Sayansi za Afya na Sayansi za Kilimo na Maji.
Aidha Mhe.Manyanya amesema
kuwa katika Mwaka wa 2015/16 Serikali ilitoa kiasi cha Tsh.bilioni 480
kugharamia Mikopo pamoja na ruzuku kwa wanafunzi wapatao 124,358.
Ameongeza kuwa Serikali inalifanyia kazi suala la wanafunzi
kutopata Mikopo ili kuongeza idadi ya
wanafunzi.
Imetolewa na:
Idara
ya Habari-MAELEZO.
0 comments:
Post a Comment