Jovina Bujulu-MAELEZO.
Tanzania
ni miongoni mwa nchi 193 zilizosaini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa
kupambana na kuenea hali ya jangwa duniani (UNCCD). Mkataba huu unalenga
kupambana na tatizo la uharibifu wa ardhi katika maeneo yenye ukame na
kufanya juhudi za kuyahifadhi.
Mkataba
huu ni muhimu kwa nchi yetu ambayo uchumi wake unategemea ardhi kwa
ajili ya kilimo ambacho kinachochea maendeleo na ajira kwa wananchi
walio wengi.
Hivi
karibuni dunia iliadhimisha siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame ambayo ilikiongozwa na kauli mbiu isemayo “Ardhi ni
makazi yetu tuitunze kwa manufaa ya baadaye”. Kauli mbiu hii
inahamasisha jamii kutunza ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu.
Akiongea
hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba alisema kuwa kauli mbiu hii
inahimiza jamii kuongeza juhudi za kutunza ardhi, na kuzingatia
maendeleo endelevu ya rasilimali tulizo nazo kwa ajili ya maendeleo ya
sasa na kwa vizazi vijavyo.
Madhumuni
ya kuadhimisha siku hii ni pamoja na kuongeza uelewa miongoni mwa jamii
na kujua athari za jangwa na ukame katika maisha ya kila siku ya
binadamu na jinsi ya kuthibiti hali hiyo.
“Malengo
hayo yanadhihirisha umuhimu wa utunzaji wa ardhi na udongo kwa matumizi
endelevu hasa kwa ajili ya kilimo, mifugo, na huduma nyingine kama
utalii wa wanyama pori na uwindaji.” Aliongeza Mhe. Makamba.
Umuhimu
wa kutunza ardhi pia unaonekana katika kuhifadhi vyanzo vya maji na
miti ili kuwezesha shughuli za uzalishaji mali na uwekezaji katika
viwanda ili kuleta ustawi wa jamii.
Hali
ya uharibifu wa ardhi na vyanzo vya maji imeongezeka kwa kasi na
kuongeza ukame, upungufu wa mazao ya kilimo na kuongeza umaskini
miongoni mwa jamii.
Takwimu
zinaonesha kuwa asilimia 61 ya eneo la nchi yetu liko hatarini kugeuka
jangwa. Hali hii ni tishio kubwa kwa maendeleo ya nchi kwani uwepo wa
jangwa ni kikwazo kikubwa kinachosababisha kushuka kwa uchumi, hasa
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Tanzania
ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa kwa kiasi kikubwa na hatari ya
kuenea kwa jangwa na ukame. Waziri Makamba aliitaja mikoa mbayo iko
katika hatari kubwa ya kugeuka jangwa kuwa ni pamoja na Singida, Dodoma,
Shinyanga, Geita, Simiyu, Manyara na baadhi ya maeneo ya mkoa wa
Arusha.
Madhara
ambayo yameanza kuonekana ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji
katika maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na wanyama pori, upungufu wa
mvua kutokana na kukata miti holela, kupungua kwa maeneo ya kilimo na
malisho ya mifugo.
Aidha,
jangwa na ukame vinasababisha tabaka la juu la ardhi kuwa wazi na hivyo
kusababisha mmomonyoko wa udongo, hali ambayo inapunguza rutuba na
hivyo kupunguza uzalishaji wa mazao kwa kiasi kikubwa.
Pamoja
na kuwepo kwa hatari ya kuwepo kwa jangwa na ukame, Serikali ya Awamu
ya Tano inafanya jitihada kubwa za kukabiliana na janga hilo kwa
kusimamia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017 hadi
2020/2021 ili kusimamia maliasili, mazingira na mabadiliko ya tabia
nchi.
Malengo
ya mpango huu ni pamoja na kuhakikisha kuwa mchango wa pato la taifa
unaotokana na matumizi endelevu ya misitu, maji, na rasilimali za bahari
linafikia asilimia 10, ongezeko la eneo la misitu kwa hekta 130,000,
upandaji wa miti 100,000,000 kwa nchi nzima ifikapo 2020.
Hatua
za kimkakati za mpango huo ni pamoja na kulinda, kurejesha na
kuhamasisha matumizi endelevu ya mifumo ya mazingira ya nchi kavu na
misitu ili kukabiliana na jangwa na shughuli zinazosababisha jangwa.
Mikakati
mingine pamoja na kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa kupambana na
kuenea kwa hali ya jangwa na ukame wa mwaka 2014 hadi 2018 ambao
unahusisha programu za upandaji miti, kuandaa mpango wa matumizi bora ya
ardhi, kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa, ufugaji bora na wa
kisasa na kuanzisha maeneo ya hifadhi na kulinda yaliyopo.
Kwa
upande wa ushiriki wa wananchi katika kukabiliana na hali hii, mkakati
huu utatekelezwa kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya, na taasisi, na
utamshirikisha kila mwananchi.
Lengo
ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani ikiwa ni pamoja na
kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika mikakati na kampeni
zilizopita, pamoja na motisha na ushiriki wa sekta binafsi. Mkakati huu
umeanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo.
Serikali
pia imeweka mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwaelekeza
shughuli nyingine za uzalishaji mali ili waepuke utegemezi wa maliasili
ya misitu ambapo programu ya upandaji miti ya mwaka 2016 hadi 2021
inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 kila mwaka hasa katika maeneo
yaliyo katika hatari zaidi ya kugeuka jangwa.
Mikakati
yote hii itafanikiwa endapo kila mwananchi atakuwa sehemu ya kupunguza
kuenea kwa tatizo hilo kwa kuzingatia matumizi endelevu ya ardhi.
Matumizi
hayo ni pamoja na kupanda na kutunza miti ambako kutasaidia ulinganifu
katika shughuli za kilimo, ufugaji, misitu, uhifadhi wa vyanzo vya maji
na kuhakikisha mifumo ya ikolijia inategemeana na haiingiliwi.
Ni
wakati sasa muafaka kwa wananchi kuunga mkono wito wa Mhe. Makamba
kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka 2017 ya siku
ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ili kutunza ardhi kwa
vizazi vijavyo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment