Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi
Juliana Pallangyo (kulia) akiwa katika kikao na Balozi wa Tanzania nchini
Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro (kushoto), Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma
Julai 24, 2017. Wengine pichani ni wataalam wa Wizara na Taasisi zake
walioshiriki kikao hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo (katikati), akiongoza kikao cha wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi
zake na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha Rose Migiro (kushoto kwa
Naibu Katibu Mkuu.)
Balozi wa Tanzania
nchini Uingereza, Dkt. Asha Rose Migiro (mwenye Koti la Pinki) na Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt.
Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia kwa Balozi), wakiwa katika picha ya pamoja na
wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi zake, Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo (kulia), akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt.
Asha-Rose Migiro, Kitabu cha Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme
(Power System Master Plan). Wanaoshuhudia ni wataalam wa Wizara pamoja na
Taasisi zake.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kushoto),
akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro (kulia),
baada ya kikao baina yao Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Julai 24 mwaka
huu.
Na
Veronica Simba – Dodoma
Kufuatia Kongamano
kubwa la Uwekezaji linalotarajiwa kufanyika nchini Uingereza, mwezi Septemba
mwaka huu, Balozi wa Tanzania nchini humo, Dkt. Asha-Rose Migiro amekutana na
wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake, wakiongozwa na Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kujadili fursa za
uwekezaji nchini katika sekta husika.
Katika kikao hicho
kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Julai 24 mwaka huu, Balozi
Migiro, alisema kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza umejipanga kulitumia
vema kongamano hilo ambapo watanadi fursa za uwekezaji katika sekta zote muhimu
nchini, zikiwemo za nishati na madini.
“Ni kwa sababu hiyo,
nimeona nifike hapa ili nikutane nanyi, tujadili kuhusu fursa za uwekezaji hapa
nchini katika sekta za nishati na madini ili tuweze kuzinadi wakati wa
kongamano hilo,” alisema Balozi Migiro.
Akifungua majadiliano
baina ya wataalam hao na Balozi Migiro, Naibu Katibu Mkuu Pallangyo,
alibainisha kuwa zipo fursa nyingi za uwekezaji hapa nchini, katika sekta za
nishati na madini na kupongeza hatua ya Balozi Migiro kudhamiria kuzinadi fursa
hizo kwa wawekezaji nchini Uingereza.
Aidha, kwa upande wa
sekta ya nishati, Dkt. Pallangyo alimwomba Balozi Migiro kupeleka maombi kwa
Serikali za Uingereza na Ireland kusaidia miradi ya usambazaji umeme vijijini
inayoendelea nchini kote.
Akizungumzia fursa za
uwekezaji zilizopo katika sekta ndogo ya umeme, Mhandisi Nishati, Christopher
Bitesigirwe alibainisha kuwa mpango wa serikali ni kuzalisha umeme hadi kufikia
megawati 5000 ifikapo mwaka 2020 hivyo wawekezaji makini wanaendelea
kukaribishwa.
Mhandisi Bitesigirwe
alieleza kuwa, vyanzo vilivyoainishwa kwenye Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa
Sekta Ndogo ya Umeme ni pamoja na gesi asilia, maji, makaa ya mawe na nishati
jadidifu (jua, upepo, jotoardhi na tungamotaka).
Kwa upande wa miradi
ya usafirishaji wa umeme, alitaja fursa zilizopo kuwa ni pamoja Mradi wa
kusafirisha umeme kuanzia Mbeya hadi Nyakanazi (North West transmission line)
wa kilovoti 400, Iringa hadi Mbeya (KV 400), Chalinze hadi Dodoma (KV 400) na
SomangaFungu hadi Kinyerezi (KV 400).
Vilevile, Mhandisi
Bitesigirwe alitaja fursa iliyopo katika Miradi ya Usambazaji Umeme kuwa ni
uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji umeme.
Naye Mjiolojia Mkuu
kutoka Idara ya Nishati, Habass Ngulilapi, alimweleza Balozi Migiro kuwa fursa
za uwekezaji zilizopo katika sekta ndogo ya Petroli ni utafiti wa gesi asilia
pamoja na mafuta unaoendelea nchini.
“Hadi sasa mafuta
hayajagunduliwa nchini lakini kiasi cha futi za ujazo trilioni 10 za gesi
asilia, kimegunduliwa katika maeneo ya mabonde ya nchi kavu,” alisema
Ngulilapi.
Aliongeza kuwa, hadi
kufikia mwezi Aprili 2017 kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa katika maeneo
ya mabonde ya nchi kavu na katika kina cha maji mafupi na marefu ni futi za
ujazo trilioni 57.25.
Kwa upande wake,
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, akizungumzia fursa za
uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini, aliitaja miradi ya uongezaji thamani
madini ya aina mbalimbali hapa nchini.
Mhandisi Mulabwa
alibainisha kuwa, Mitambo ya kuchenjulia madini ya metali inahitajika sana kwa
sasa hapa nchini ili kuwezesha kuchenjua madini hayo nchini pasipo
kuyasafirisha nchi za nje, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
“Tayari wapo
wawekezaji mbalimbali ambao wameonesha nia kuwekeza nchini kwa kuleta mitambo
hiyo lakini kulingana na uhitaji na umuhimu wake, serikali bado inakaribisha wawekezaji
wengine mbalimbali wenye nia ya dhati, waje kuwekeza katika eneo hilo,”
alifafanua.
Aidha, Mhandisi
Mulabwa, alibainisha fursa nyingine ya uwekezaji iliyopo katika sekta ya madini
kuwa ni kuongeza thamani mawe mbalimbali ya vito kwa kuyakata na kuyang’arisha.
Akifafanua zaidi,
alieleza kuwa, kuanzisha viwanda vya kutengeneza mapambo mbalimbali
yanayotokana na madini ya vito na metali hapa nchini, ni fursa adhimu ambapo
Serikali inawakaribisha wawekezaji makini kuja kuwekeza katika sekta hiyo.
Kaimu Meneja wa
Uwekezaji kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Nsalu Nzowa, alimweleza
Balozi Migiro kuwa, fursa zilizopo kupitia shirika hilo ni kuendeleza Mradi wa
kuchimba madini ya dhahabu wa Buhemba ambao ulikuwa ukitekelezwa kwa ubia kati
ya Jeshi la Tanzania na la Afrika ya Kusini, na baadaye kusimamishwa.
Vilevile, alitaja
fursa nyingine ya uwekezaji kuwa ni uchimbaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya
matumizi katika viwanda vya saruji pamoja na matumizi mengine mbalimbali.
Kwa upande wa Wakala
wa Jiolojia Tanzania (GST), Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kijiolojia, Maruvuko
Msechu, alimweleza Balozi Migiro kuwa Wakala huo unaendesha uchunguzi na tafiti
mbalimbali za kijiolojia, ambazo zinahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau
mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa
Kanzidata wa GST, Yokbeth Myumbilwa, alieleza kuwa, wawekezaji wanashauriwa
kutembelea Tovuti ya Wakala huo ili kujipatia maelezo kuhusu tafiti mbalimbali
zilizofanywa na Wakala zitakazowasaidia kupata uelewa wa aina mbalimbali za
madini yanayopatikana nchini pamoja na maeneo yanakopatikana.
0 comments:
Post a Comment