Imeandikwa na Magnus Mahenge, Dodoma.
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kuwavua uanachama wabunge wanane na
madiwani mawili, Spika wa Bunge, Job Ndugai amekiri kupokea barua kuhusu
uamuzi huo, na anatafakari kabla ya kutoa uamuzi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 71 (f) chama
cha siasa kina mamlaka ya kumsimamisha uanachama na hivyo anapoteza haki
ya kuwa mbunge kupitia chama hicho. Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Ndugai alisema ataitafakari na kuifanyia kazi barua hiyo na
ataitolea taarifa baadaye.
“Suala la kuwaondoa uanachama ni la utashi wa vyama vyenyewe, na kila
chama kina utaratibu wake, hivyo bado naendelea kuitafakari barua hiyo
na uamuzi kuhusu wabunge waliofukuzwa uanachama nitautolea baadaye,”
alisema Spika Ndugai (pichani).
Profesa Lipumba alisema Dar es Salaam jana kuwa mbali na wabunge hao,
Baraza la Uongozi la chama pia limewavua uanachama madiwani wawili wa
Viti Maalumu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa makosa ya kinidhamu tangu
Julai 24, mwaka huu.
Aliwataja wabunge kuwa ni Riziki Shahali Ngwali, Saverina Mwijage,
Salma Mwassa, Saumu Sakala, Riziki Lulida, Mgeni Jadi Kadika, Raisa
Abdallah Mussa, Miza Bakari, Halima Ali Mohammed na Khadija Al Kassim.
Madiwani waliovuliwa nyadhifa zao ni Diwani Viti Maalumu, Leila
Hussein Madibi (Ubungo) na Diwani wa Viti Maalumu, Elizabeth Magwaja
(Temeke). Wabunge na madiwani hao wanatuhumiwa kutokana na kitendo cha
kupewa na kupokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe na kula njama za kukihujumu CUF kwa kushiriki katika operesheni
iliyoandaliwa na Chadema iliyoitwa ‘Ondoa Msaliti Buguruni’, jambo
linalokiuka Katiba ya CUF ya 1992.
Pia wabunge na madiwani hao walikihujumu chama hicho katika uchaguzi
wa marudio wa madiwani uliofanyika Januari 22, mwaka huu. Pia waliruhusu
na kuipa fursa Chadema kuwa msemaji wa masuala ya CUF, kinyume cha
matakwa ya Katiba yao na kulipia pango na kufungua ofisi ya chama
Magomeni bila kufuata taratibu za kikatiba.
Pia inaonesha kwamba wanatuhumiwa hao, walichangia fedha zilizotumika
kukodisha mabaunsa kwa lengo la kuwadhuru viongozi watiifu wa chama
upande wa Lipumba, Sakaya na Mkurugenzi wa CUF wa Mambo ya Nje na Mbunge
wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma.
Profesa Lipumba alisema kabla ya kuvuliwa uanachama, waliitwa mbele
ya Kamati ya Maadili wao waliosusia mwito huo wa kwenda kujieleza juu ya
tuhuma zinazowakabili za kula njama na Chadema ili kuweza kumwondoa
yeye madarakani.
Wabunge na madiwani hao walisusia mwito hata baada ya kupewa barua za
kuitwa na Kamati ya Maadili, hivyo Baraza Kuu limechukua maamuzi kwa
kufuata Katiba yake ya mwaka 1984 kuwafuta uanachama.
Aidha, Lipumba alisema taarifa kuhusu uamuzi huo tayari zimeshatumwa
kwenda kwenda Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye amethibitisha
kuipata barua na ameahidi kuitafakari na kuitolea uamuzi baadaye na kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya hatua zaidi.
Profesa Lipumba alisema wabunge 10 hao walioitwa na kuhojiwa na
Kamati ya Maadili ya CUF na kugomea mwito huo ni wale wanaomuunga mkono
Katibu Mkuu, Maalim Seif.
Historia ya chama hicho inaonesha kwamba hiyo si mara ya kwanza
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, kuwafukuza wanachama kwani
Januari 4, mwaka 2012, lilimfukuza uanachama aliyekuwa Mbunge wa Wawi,
Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mbunge huyo kuingia kwenye msuguano
mkubwa na Katibu Mkuu ambaye pia wakati huo alikuwa Makamu wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi, Maalim Seif Sharif Hamad.
Hamad Rashidi baada ya kuondolewa wanachama, alisikika akisema tatizo
kubwa hapa katika siasa za Kitanzania ni kwamba “viongozi wetu wa juu
hawataki kupata changamoto kutoka kwa waandamizi wao kwani hawako tayari
kuona mawazo kupingwa.”
Pamoja na Hamad Rashid ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu,
wengine waliofukuzwa ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma, Juma Said
Sanani na Yasini Mrotwa.
Mbunge huyo Hamad Rashid Januari 10, 2013, na wenzake 10
waliwasilisha maombi madogo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
wakiiomba itamke kuwa uamuzi wa Baraza la Uongozi Taifa la chama hicho
uliomvua uanachama yeye na wenzake ni batili na haikufanya hivyo.
CHANZO HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment