Imeandikwa na Anastazia Anyimike, Dodoma
BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, na
sasa sheria imetamka kuwa ofi sa wa umma aliyesababishia serikali au
taasisi ya umma kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa makusudi au kwa
uzembe, atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kukatwa mshahara wa miezi
sita.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju amesema mabadiliko
ya Sheria ya Bajeti na yale ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
yaliyopitishwa jana bungeni, hayakusudii kupoka kwa namna yoyote ile
mamlaka ya kisheria ya Bunge.
Kifungu cha 65(2) cha Sheria ya Bajeti kinaweka masharti kuwa iwapo
itathibitika kuwa ofisa wa umma kwa makusudi au kutokana na uzembe,
alisababisha serikali au taasisi ya umma kushindwa kutekeleza majukumu
yake chini ya sheria hiyo, atatenda kosa la kinidhamu.
Masaju alisema atawajibishwa binafsi kwa kuchukuliwa hatua za
kinidhamu au kushtakiwa kwa kosa la jinai kulingana na aina ya madhara
yatokanayo na kushindwa majukumu hayo.
Kuhusu uhamisho wa fedha, alisema baada ya mabadiliko hayo hivi sasa
uwasilishaji wa taarifa za uhamisho wa fedha na uwasilishaji wa taarifa
za serikali na taarifa za mapato na matumizi, zitawasilishwa kila baada
ya miezi sita kwa maana ya nusu mwaka, badala ya miezi mitatu kwa maana
ya robo mwaka kama ilivyokuwa awali.
Akihitimisha hoja yake aliyoiwasilisha bungeni kuhusu Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017, ambayo ndani
yake ililenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya Bajeti na mabadiliko
ya sheria ya ofisi yake, Masaju alisema kimsingi muswada huo sio wa
kubadilisha kanuni za haki na madaraka ya Bunge wala madaraka ya Kamati
ya Bajeti kama baadhi ya wabunge wanavyodhani
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment