Na: Lilian Lundo - MAELEZO.
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere kinatarajia kufundisha programu ya uongozi maadili na utawala bora kwa
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo watasoma kwa awamu,
mara baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti.
Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano
Mwandamizi wa Chuo hicho, Evelyne Mpasha leo jijini Dar es Salaam katika
maonesho ya saba saba ya 41 yanayoendelea
Jijini humo.
Alisema Chuo hicho kimejizatiti kurejesha
maadili kwa viongozi na Watanzania kupitia programu ya uongozi ya maadili na
utawala bora inayotolewa chuoni hapo.
Mpasha amesema, Chuo hicho
kilianzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961
kikiwa na lengo la kufundisha viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM)
maadili na uzalendo kwa nchi.
"Tangu kuanza mfumo wa vyama
vingi nchini, Chuo kimekuwa kikijihusisha na utoaji wa programu za kitaaluma na
kuanzia mwaka 2015 chuo kimerejesha tena
kozi ya uongozi na maadili," amesema Mpasha.
Amesema kuwa, kozi hiyo hutolewa kwa
viongozi walio katika ngazi ya maamuzi kutoka Taasisi za Umma na Binafsi ambapo
hufundishwa masuala ya uzalendo, utaifa na maendeleo ya nchi.
Aidha, amesema Chuo kimepokea
viongozi mbalimbali kutoka katika Halmashauri mbalimbali, Taasisi za Serikali
na zisizo za Kiserikali kwa ajili ya kujifunza programu hiyo.
Nae, Mhadhiri wa Chuo hicho,
Tiberius Mlowosa amesema kumekuwepo na viongozi wengi wanao hujumu uchumi
wa nchi kutokana na kukosa mafunzo ya uongozi na maadili.
"Kama viongozi wote walio ngazi
ya maamuzi wangepata mafunzo ya uongozi maadili na utawala bora, tusingekuwa na
masuala ya EPA wala ESCROW," amesema Mlowosa.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere kinatoa programu nyingine nje ya programu hiyo ya uongozi ambazo ni
Utawala na Rasilimali Watu, Usimamizi wa Biashara, Maendeleo ya Jamii, Uhasibu,
Ununuzi na Ugavi kuanzia ngazi ya cheti .
0 comments:
Post a Comment