SERIKALI imetangaza kuwa viwanda 10 vilivyokuwa vimeshindwa kuzalisha
au kuendelezwa, vimefutiwa umiliki wake na kupewa wawekezaji wengine
kuvifufua. Aidha, viwanda 11 kati ya 56 vilivyokuwa vimefungwa,
vimefufuliwa vitaanza uzalishaji wake wakati wowote.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage alitaja viwanda 10 ambavyo wamepewa wamiliki
wengine kutokana na umiliki wa awali kufutwa kuwa ni Kiwanda cha Mkata
Saw Mills, Kiwanda cha Korosho Lindi na Kiwanda cha Taifa cha Chuma na
Manawa Ginnery.
“Kiwanda cha Tembo Chipboard, Mang’ula Mechanical Tools, Mgodi wa
Pugu Kaolin, Dabaga Tea Factory, Kiwanda cha Polysack na Kiwanda cha
Kilimanjaro Textile Mills cha Arusha,” alivitaja Mwijage ikiwa ni siku
chache baada ya kubanwa na Rais John Magufuli kuchukua hatua dhidi ya
wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda miaka 20 tangu serikali
ilipovibinafsisha.
Alivitaja viwanda vitano kati ya 11 ambavyo wamiliki wengine wamepewa
kuvifufua ni Kiwanda cha Mvinyo Dodoma (DOWICO), Kiwanda cha Mafuta
Morogoro (MOPROCO), Tabora Textile Mills, Manonga Ginnery na kilichokuwa
Kiwanda cha Viatu Morogoro.
Katika orodha hiyo, pia alivitaja viwanda vinne ambavyo vinafufuliwa
na wawekezaji wapya baada ya wawekezaji wa awali kutovifufua ni Morogoro
Canvas Mills (TSSA), Mwanza Textile Mills (TSSA), Kiwanda cha Nguo cha
Urafiki (TSSA) na Kiwanda cha Mutex (LAPF).
Mwijage alitaja viwanda viwili vinakusudia kufufuliwa na tayari
mipango ya uwekezaji, imewasilishwa na vipo katika uangalizi wa miezi
mitatu kuanzia Agosti 10, mwaka huu ni pamoja na Kiwanda cha Korosho
Kibaha na Newala I Cashewnuts Factory.
Alisema viwanda vitano vipo katika uangalizi hadi Agosti 22, mwaka
huu, ambapo serikali itachukua hatua dhidi yake kuanzia wakati huo
ambavyo ni Sabuni industries Limited, Tanzania Moshi Pesticides,
Tanzania Bag Corporation, Ilemela Fish Processing Plant na Mzizima Maize
Mill.
Mwijage alisema ubinafsishaji nchini, ulihusisha viwanda, mashamba,
kampuni za biashara, hoteli na kampuni za usafirishaji zipatazo 431, na
kati yake, viwanda vilikuwa 156 ambavyo 62 vinafanya kazi vizuri, 28
vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 10 vilibinafsishwa kwa kuuzwa
mali moja kwa moja.
Alisema katika orodha hiyo, Kiwanda cha Mwanza Tanneries ambacho
hakijaendelezwa tangu kubinafsishwa miaka ya 1990, mwekezaji wake
ameamua kukirudisha serikalini.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment