Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amezitaka Halmashauri za
Wilaya, Mji na Manispaa Mkoani Dodoma kuhakikisha zinatenga asilimia
kumi (10%) ya makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na
Walemavu kuanzisha miradi ya viwanda vidogo na vya kati.
Lengo
ni kuitikia kampeni ya Serikali inayoitaka Mikoa kuanzisha viwanda kama
ilivyozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI
Mheshimiwa Seleman Jafo.
Akizungumzia
hilo, ameonya tabia ya baadhi ya Halmashauri kutotoa asilimia kumi
(10%) ya makusanyo yake ya ndani au kutoa kiasi kidogo kwa ajili ya
vijana, wanawake na walemavu na kuwa utaratibu unaotumika sasa wa
Halmashauri kukopesha fedha hizo wakati mwingine sio muafaka sana badala
yake Halmashauri zitumie fedha hizo kuwafungulia vijana, wanawake na
walemavu viwanda vidogovidogo na kuwakabidhi waendeleze uzalishaji na
kuviendesha.
Dkt.
Mahenge amebainisha hayo wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya
kutembelea Wilaya za Mkoa wa Dodoma kujitambulisha na kukagua miradi ya
maendeleo ambapo amesema kuwa viwanda vinavyoweza kuanzishwa ni vya
uchakataji wa nafaka, usindikaji mazao na utengenezaji vyakula vya
Mifugo.
Amesema
kuwa asilimia kumi hiyo ikitumika na kusimamiwa vizuri inaweza
kutekeleza kampeni ya kuanzisha viwanda ambapo vijana na wanawake
wanaweza kufaidika kuanzia ngazi za chini kama vijijini kwa kupata ajira
kipato na halmashauri kupata ushuru.
Aidha,
ameongeza kuwa mbali na uanzishaji viwanda miradi mingine Halmashauri
inayoweza kuwaanzishia vijana, wanawake na walemavu ni pamoja na ufugaji
samaki kwa kuwachimbia mabwawa.
Ametaja
miradi mingine mbali na viwanda kuwa Halmashauri zinaweza kuchimba
visima na kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili vijana, wanawake na
walemavu waendeshe kilimo cha umwagiliaji kuzalisha mazao mbalimbali
ambayo yanaweza kuwa malighafi kwenye viwanda vinavyoanzishwa.
“Sisi
ni Viongozi, maana ya kuwa viongozi ni pamoja na kuwasaidia wananchi
kuweza kufanya maamuzi yenye manufaa kwao na uanzishwaji wa viwanda
utawanufaisha wananchi wengi na Mkoa kwa ujumla” alimalizia Dkt.
Mahenge.
0 comments:
Post a Comment