Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
HOTUBA
YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHE. DKT. PHILIP ISDOR MPANGO (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA
MWAKA 2018/19 NA MWONGOZO
WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI
KWA MWAKA 2018/19
DODOMA NOVEMBA, 2017
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae
kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango
na Bajeti kwa Mwaka 2018/19.
2. Mheshimiwa Spika, awali
ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima
na afya. Aidha, tunamshukuru sana kwa kuendelea kulijalia Taifa letu
amani na utulivu na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa tisa wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya
kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
3. Mheshimiwa Spika,
kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuongoza
Wizara ya Fedha na Mipango kufuatia mabadiliko aliyoyafanya hivi
karibuni katika Baraza lake la Mawaziri na safu ya uongozi wa Mikoa.
Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa
Mikoa waliobakia katika nafsi zao na wale waliobadilishwa vituo vya
kazi. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati wote walioteuliwa kuwa
Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa wapya.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii adhimu kutambua na
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na makini katika
kusimamia rasilimali za Taifa, kupambana na rushwa, kuimarisha nidhamu
na uwajibikaji katika utumishi wa umma na zaidi ya yote, kwa moyo wake
adili katika kupatia majibu kero za wanyonge. Hakika uongozi wake
umezidi kuijengea heshima kubwa nchi yetu.
5. Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Janeth Masaburi (Mb)
aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu
hivi karibuni kutoka Chama Tawala cha CCM. Aidha, nawapongeza kwa pamoja
Waheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Kiza Hussein Mayeye, Nuru Awadh
Bafadhili, Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Sonia Jumaa
Magogo,
Rehema Juma Migilla na Zainab Mndolwa Amir walioteuliwa na Chama cha
Wananchi - CUF kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ninapenda kuwakaribisha na kuwashauri watumie jukwaa hili kikamilifu
katika kuishauri Serikali na kuwatumikia wananchi. Napenda pia
kumpongeza Bw. Stephen Kagaigai kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa
Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.
Mheshimiwa Spika, ninawiwa pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb) na
watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu,
Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya
hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo. Aidha,
ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na
wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha
Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.
7. Mheshimiwa Spika,
hoja ninayoiwasilisha hapa imetayarishwa kwa kuzingatia dhana ya
ushirikishwaji mpana wa jamii. Kwa ujumla tumepata maoni na ushauri
kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii na Taasisi za Serikali. Siwezi
kuwataja mmoja mmoja wale wote waliochangia hoja hii hadi kufikia hapa.
Hata hivyo, kwa namna ya kipekee, napenda kuishukuru na kutambua
mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake
Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini katika
kuboresha rasimu za Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka
2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka
2018/19. Maoni na ushauri mahsusi wa Kamati ulijikita katika maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na yafuatayo:
(i) Kujumuisha matumizi
ya gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na kama malighafi katika
viwanda ikiwemo viwanda vya mbolea;
(ii) Kuzingatia maeneo
yanayogusa wananchi walio wengi kwa ajili ya kukuza kipato na kupunguza
umaskini hususan kilimo, uvuvi, upatikanaji wa pembejeo na mitaji;
(iii)
Kuweka msukumo mkubwa katika kuboresha mazingira kwa ajili ya ushiriki
wa Sekta Binafsi katika kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo
inayolenga kutimiza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu;
(iv) Kuendelea kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya;
(v) Kuendelea kulipa madeni yaliyohakikiwa na kuzuia uzalishaji wa madeni mapya; na
(vi)
Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) kwa kipindi cha miaka miwili ya awali.
8.
Mheshimiwa Spika, hoja ninayowasilisha leo mbele ya Bunge lako Tukufu
ni hatua ya awali katika mchakato wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2018/19. Madhumuni ya wasilisho hili ni kuomba maoni
na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wakiwa ndiyo wawakilishi wa sauti za
wananchi kuhusu masuala yanayostahili kupewa kipaumbele na msisitizo
katika Mpango na Bajeti kwa mwaka ujao. Hivyo, napenda kuahidi kuwa
maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Bajeti na yote
yatakayotokana na Bunge lako Tukufu linapokaa sasa kama Kamati ya
Mipango tutayazingatia kwa dhati wakati wa kuandaa Mpango wa Maendeleo
wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19.
9.
Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka
2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19
yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2015; Sera na
mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kisekta, kikanda na kimataifa; na
Maelekezo mengine ya Serikali. Aidha, vyote vimezingatia hali halisi ya
mwenendo wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2016 na nusu ya kwanza ya
mwaka 2017. Pia, vimezingatia mahitaji ya msingi katika kuimarisha kasi
ya utekelezaji wa Mpango na kujenga mazingira yatakayowezesha kufikiwa
kwa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda kama ilivyobainishwa
katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
10. Mheshimiwa
Spika, hoja ninayoiwasilisha ina vitabu viwili. Kitabu cha kwanza
kinahusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19.
Kitabu cha pili kinawasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo
wa Taifa kwa Mwaka 2018/19. Vitabu vyote viwili vinapaswa kusomwa kwa pamoja.
MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2018/19
11.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa kuwasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya
Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19. Mwongozo huu unaainisha maelekezo
mahsusi yanayopaswa kuzingatiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea,
Taasisi na Wakala wa Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuandaa, kutekeleza, kufuatilia,
kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka
2018/19.
12. Mheshimiwa Spika, lengo la Mwongozo wa
Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19 ni kuwaelekeza Maafisa
Masuuli kuhusu maeneo ya kipaumbele na masuala mahsusi yanayopaswa
kupewa msukumo wa kipekee katika uandaaji wa mipango na bajeti za
mafungu husika. Maelekezo haya yanatokana na Sheria ya Bajeti Na. 11 ya
mwaka 2015 na Kanuni zake; maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya
kibajeti, ukusanyaji wa mapato, usimamizi na udhibiti wa matumizi;
usimamizi wa mashirika na taasisi za umma; na usimamizi wa madeni ya
Serikali. Mwongozo pia umeainisha mfumo wa bajeti ya mwaka 2018/19,
ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya awali ya mfumo wa mapato na matumizi
ya Serikali kwa mwaka 2018/19 na mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na
utoaji taarifa za utekelezaji.
Mapitio ya Viashiria vya Uchumi kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2017
13.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwasilisha vipengele muhimu vya Mwongozo,
naomba nianze kueleza kwa kifupi mapitio ya viashiria vya uchumi kwa
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017 na utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2016/17.
14. Mheshimiwa Spika, viashiria vya
mwenendo wa uchumi kwa ujumla wake vinaonesha kuwa uchumi wa Taifa ni
imara. Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017, Uchumi wa Taifa
ulikua kwa asilimia 6.8, ukichangiwa
zaidi na kuimarika kwa sekta
za mawasiliano, usafirishaji na ujenzi. Ukuaji wa sekta ya kilimo
uliongezeka kutoka wastani wa asilimia 2.7 nusu ya kwanza ya mwaka 2016
hadi kufikia asilimia 3.1 nusu ya kwanza ya mwaka 2017 kutokana na hali
nzuri ya hewa.
15. Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa Bei bado
umeendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja kutokana na kuongezeka
kwa ugavi wa chakula katika masoko ya ndani na ya nchi jirani; kutoyumba
kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia; na utekelezaji wa
sera za bajeti za kupunguza matumizi yasiyo na tija. Mfumuko wa bei
mwezi Julai ulikuwa asilimia 5.2, Agosti asilimia 5.0 na Septemba
asilimia 5.3 ikilinganishwa na lengo la asilimia 5 hadi 8 kwa kipindi
husika. Mwenendo wa Thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya
Marekani uliendelea kuwa imara katika kipindi chote cha mwaka 2016/17
narobo ya kwanza ya 2017/18. Thamani ya shilingi ya Tanzania imebadilika
kutoka shilingi 2,177.26 kwa dola moja ya Marekani mwezi Januari 2016,
hadi shilingi 2,221.96 mwezi Januari 2017. Kasi ya shilingi kupungua
thamani iliongezeka na kudumu kwa muda mfupi mwezi Januari 2017 hali
iliyosababishwa na Benki Kuu ya Marekani kupandisha riba yake na hivyo
kuongeza mahitaji ya dola ya Marekani duniani kwa ajili ya kuwekeza.
Aidha, baada ya mwezi Januari 2017, thamani ya shilingi iliendelea kuwa
tulivu na kufikia shilingi 2,237.78 mwezi Oktoba 2017.
16.
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa liliongezeka kufikia dola za Marekani
milioni 26,115.2 mwezi Juni 2017, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia
17.0, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 22,320.76 katika
kipindi kama hicho mwaka 2016. Ongezeko hilo lilichangiwa na mikopo
mipya iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile:
Standard Gauge Railway; Strategic Cities; mradi wa usafirishaji Dar es
Salaam (DART) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam. Deni
hili la Taifa linajumuisha deni la Serikali lililofikia dola za Marekani
milioni 22,443.70 na deni la sekta binafsi la dola za Marekani milioni
3,671.50. Pamoja na ongezeko hili, viashiria vyote bado vinaonesha kuwa
deni la Taifa ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Uwiano kati ya deni na Pato la Taifa umefikia asilimia 31.2
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.
Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti 2016/17
17.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitekeleza bajeti kulingana na upatikanaji
wa mapato. Mapato yaliyopatikana kutoka vyanzo vyote kwa mwaka 2016/17
yalikuwa Shilingi bilioni 23,634.55, ikilinganishwa na makadirio ya
Shilingi bilioni 29,539.60. Mapato ya ndani yalikuwa Shilingi bilioni
16,639.97, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio lakini yakiwa na ongezeko
la asilimia 17.7 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16. Aidha,
misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia
Shilingi bilioni 2,474 sawa na asilimia 68.7 ya ahadi. Mikopo ya ndani
ilikuwa Shilingi bilioni 4,504.8 sawa na asilimia 83.8 ya lengo la
kukopa Shilingi bilioni 5,374.3. Kwa upande wa mikopo ya nje ya
kibiashara, Shilingi bilioni 1,226.8 zilipatikana, ikiwa ni asilimia
58.4 ya malengo. Kiasi cha Shilingi bilioni 1,211.0 kati ya mikopo yenye
masharti ya kibiashara hakikuweza kutumika kwa mwaka 2016/17 kwa kuwa
kilipokelewa mwishoni mwa mwaka. Kiasi hiki cha fedha kitatumika
kugharamia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa katika mwaka 2017/18.
18.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi bilioni 23,634.55 zilitolewa, ikiwa
ni asilimia 80.0 ya makadirio ya mwaka 2016/17. Kiasi hiki kilikuwa ni
zaidi ya matumizi halisi ya mwaka 2015/16 ya Shilingi bilioni 22,099.1
kwa asilimia 6.5. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 17,136.2
zilitumika kwa matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 96.7 ya lengo na
Shilingi bilioni 6,498.3, kwa matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia
55.0 ya lengo la mwaka.
19. Mheshimiwa Spika, kwa niaba
ya Serikali napenda kuwapongeza Watanzania walioitikia wito wa Serikali
wa kulipa kodi kwa hiari hususan ongezeko la mwitikio wa kutumia mashine
za kieletroniki (EFD). Mwaka 2016/17 tulishuhudia pia mwitikio na
hamasa ya kipekee kwa wananchi kulipa kodi ya majengo. Haya kwa ujumla
wake yanaonesha uelewa wa Watanzania kuhusu wajibu wa kulipa kodi ili
kuchangia maendeleo yao. Nawaomba Watanzania waendelee na moyo huo wa
kizalendo na kuwahimiza wale ambao hawajapata mwamko kuanza kulipa kodi
kwa hiari. Ni kwa njia hii pekee ndipo tutaweza kujenga msingi endelevu
wa uchumi na ustawi wa jamii na kulinda heshima ya uhuru wetu.
Mapitio ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2016/17
20.
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi
ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 ni pamoja na:- kugharamia ujenzi wa awamu
ya kwanza wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge kutoka Dar es
Salaam hadi Morogoro (Shilingi bilioni 1,000.0); ujenzi na ukarabati wa
barabara kwa kutumia fedha za mfuko wa barabara (Shilingi bilioni
807.4); mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (Shilingi bilioni 495.4);
elimumsingi bila malipo (Shilingi bilioni 206.9); upanuzi wa miundombinu
ya umeme vijijini (Shilingi bilioni 361.5); uboreshaji wa usafiri wa
anga kwa ununuzi wa ndege mpya mbili (Shilingi bilioni 103.4) na malipo
ya awali ya ndege mpya nne (Shilingi bilioni 320.1); uwekezaji kwenye
miundombinu ya umeme (Shilingi bilioni 176.5); ununuzi wa dawa na vifaa
tiba (Shilingi bilioni 165); uwekezaji katika miundombinu ya usambazaji
maji mijini na vijijini (Shilingi bilioni 137.4); na upatikanaji wa
pembejeo za kilimo (Shilingi bilioni 21).
21. Mheshimiwa
Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: kupata mradi
mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi
Chongoleani-Tanga (dola za Marekani bilioni 3.5) ambapo kupitia mradi
huu Taifa litanufaika na ajira, utaalamu na fursa za kibiashara. Miradi
mingine ni pamoja na:- upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam (dola za
Marekani milioni 345); ununuzi wa asilimia 35 ya hisa za ZANTEL katika
Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na hivyo kuiwezesha Serikali kumiliki
TTCL kwa asilimia 100 (Shilingi bilioni 14.9); kuimarisha ulinzi na
usalama wa raia na rasilimali za Taifa.
22. Mheshimiwa Spika, hatua za utekelezaji wa baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali na Sekta Binafsi ni kama ifutavyo:
(i)
Miradi ya sekta binafsi, hususan, ya viwanda imekuwa na mwenendo mzuri,
ambapo viwanda mbalimbali vilianza uzalishaji, ikiwa ni pamoja na
viwanda vya kuzalisha vifungashio vya Global Packaging (T) Ltd na
Madoweka Co. Ltd; viwanda vya kuzalisha bidhaa za ujenzi vya Goodwil
Ceramics Ltd na Waja General Co. Ltd; viwanda vya kuzalisha vinywaji
baridi vya Saini Food Products Co. Ltd; Sayona Drinks Ltd na kiwanda cha
kusindika nyama cha Mitoboto Farmers Co. Ltd. viwanda vyote
nilivyotaja vipo mkoa wa Pwani. Aidha, kuna kiwanda cha kusindika nyama
cha Paul
Kisivani – Arusha; na viwanda vya kuzalisha mafuta ya
kula vya Jielong Mills Ltd kilichopo Shinyanga, Mkongori Oil Mills na
Nkupa Oil Mills - vilivyopo Singida, Super Cooking Oil - kilichopo
Mwanza na Mount Meru Millers - kilichopo Mara;
(ii) Miradi mipya
1,160 ya maji katika vijiji 1,206 katika Halmashauri 148; uchimbaji
visima 11 mkoani Tabora; upanuzi wa huduma ya maji safi katika manispaa
ya Dodoma na Singida;
(iii) Hospitali ya Taifa Muhimbili:
kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa vyumba 7 vya upasuaji na kuongeza
idadi ya vyumba kufikia 20 katika jengo kuu la upasuaji; kukamilika kwa
ukarabati wa vyumba vinne (4) vya upasuaji katika jengo la watoto
pamoja na kuweka mfumo wa hewa medical gas piping; kununuliwa kwa
mashine 1 ya kisasa ya CT-Scan, mashine 14 za upasuaji (diathermy
machines), mashine 2 kubwa za usafishaji vifaa (auto clave machines),
vifaa vya usikivu (cochlear implants), mashine za kutolea huduma ya
kupandikiza vifaa vya usikivu (audiometer and ABR machine) na lifti 2
kwa ajili ya majengo ya Kibasila na Sewahaji;
(iv) Huduma ya Afya
ya Uzazi na Mtoto: kukamilika kwa ukarabati mkubwa na ujenzi wa vituo
vya afya 8 vilivyopo Kanda ya Ziwa ambapo hadi sasa vituo 171 vinatoa
huduma ya upasuaji wa matatizo yatokanayo na uzazi pingamizi pamoja na
upatikanaji wa damu salama; na ununuzi wa magari 67 ya kubebea wagonjwa;
(v) Utunzaji na Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji ambapo mipaka ya
vyanzo vya maji kumi (10) imewekwa katika mabonde ya Rufiji; Ruvuma na
Pwani ya Kusini; Ziwa Rukwa na Wami/Ruvu;
(vi) Ujenzi wa Bwawa la
Kidunda: hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa usanifu wa bwawa na
barabara ya Ngerengere – Kidunda (km 76) pamoja na sehemu ya malipo ya
fidia kwa wananchi 2,603 waliohamishwa kupisha ujenzi wa bwawa na
barabara;
(vii) Mradi wa Uchimbaji wa Visima Virefu Kimbiji na Mpera ambapo visima 15 kati ya 20 vilivyokuwa vimepangwa vimekamilika; na
(viii)
Mtandao wa Majisafi Jijini Dar es Salaam ambapo shughuli za ujenzi wa
matanki saba (7), ulazaji wa mabomba makubwa yenye urefu wa kilometa 69
na madogo ya usambazaji maji kwa urefu wa kilomita 361 umekamilika
na kuanza kuunganishiwa maji kwa wateja katika maeneo ya Mbezi, Kiluvya, Tegeta na Bagamoyo
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2017/18
23.
Mheshimiwa Spika, hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwa baadhi ya
miradi ya maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka 2017/18 ni pamoja na:
(i) Ujenzi wa bwawa na mitambo ya kuzalisha umeme -Stiegler’s Gorge: zabuni ilitangazwa ili kumpata mkandarasi wa mradi;
(ii)
Ujenzi wa Reli ya Kati: ujenzi wa kipande cha Dar - Morogoro
uliendelea, ambapo ujenzi wa kambi za Ilala, Soga na Ngerengere
unaendelea; na mkandarasi wa ujenzi wa reli hiyo kwa kipande cha
Morogoro – Makutupora amepatikana, ambapo mkataba ulisainiwa Septemba,
2017;
(iii) Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi:
Ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 7 kwa kiwango cha changarawe
kutoka barabara kuu ya Dodoma – Morogoro inayoingia katika kiwanda cha
kuzalisha sukari cha Mbigiri; kununuliwa kwa matrekta 3; na kukamilika
kwa usafishaji wa shamba kubwa (ekari 1000) ambapo ekari 320 zimepandwa
miwa. Aidha, ujenzi wa majengo ya kiwanda cha sukari unaendelea;
(iv)
Kuzinduliwa kwa meli mbili (2) za mizigo katika ziwa Nyasa na ujenzi wa
kivuko kikubwa kati ya Kigongo na Busisi unaendelea;
(v) Ujenzi wa barabara zikiwemo flyovers unaendelea na barabara ya KIA – Mererani (km 26) imekamilika na kuzinduliwa;
(vi)
Hifadhi ya Mazingira na Vyanzo vya Maji: kuvitambua, kuviwekea mipaka
na kuvitangaza vyanzo vya maji 78 kuwa maeneo tengefu;
(vii)
Huduma ya Maji Vijijini: kukamilika kwa ujenzi wa miradi 90 ya maji
vijijini na hivyo kufanya jumla ya miradi iliyokamilika kufikia 1,423;
ujenzi wa jumla ya vituo vya maji 117,190;
(viii) Mradi wa Maji
wa Same – Mwanga – Korogwe: kukamilika kwa asilimia 26.3 ya mradi
ikiwemo ujenzi wa chanzo; mtambo wa kusafisha maji; na tanki la kuhifadh
i
kwa Vijiji 100 Vinavyopitiwa na Bomba Kuu kutoka Ziwa Victoria, ambapo
miradi ya vijiji 14 na upimaji na usanifu wa miradi ya vijiji 32
umekamilika; n
(x)
Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza Majisafi Dar es Salaam:
ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 77 umekamilika katika maeneo
ya Mbezi na Kiluvya.
Uwekezaji wa Sekta Binafsi
24.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutambua mchango wa Sekta Binafsi kwa
kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kuendeleza viwanda na hivyo
kuinua maisha ya watanzania. Katika Mwaka 2016, Kituo cha Taifa cha
Uwekezaji kilisajili miradi 345 na kati ya hiyo, miradi 103 ni ya
wawekezaji wa ndani, 137 ya wageni na 105 ya Ubia kati ya wawekezaji wa
ndani na wageni. Thamani ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2016 ilikuwa ni
dola za Marekani bilioni 5.92. Mgawanyiko wa miradi kisekta unaonesha
kuwa sekta ya nishati ilisajili miradi yenye thamani ya dola za Marekani
bilioni 2.46 majengo na biashara bilioni 1.13; uzalishaji viwandani
bilioni 0.62; kilimo bilioni 0.5; usafirishaji mizigo bilioni 0.38;
mawasiliano bilioni 0.28; maliasili bilioni 0.26; na bilioni 0.29 katika
sekta zingine. Aidha, sekta ya uzalishaji viwandani iliongoza kwa
kuvutia wawekezaji wengi ambapo mwaka 2016 ilisajili miradi 178
ikifuatiwa na majengo ya biashara iliyosajili miradi 48; utalii miradi
33 na kilimo miradi 24.
Changamoto za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti na Hatua za kukabiliana Nazo
25.
Mheshimiwa Spika, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na: uvujaji wa
mapato; mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa hiari; udhaifu katika ukusanyaji
wa mapato kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za
Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma;
kutopatikana kwa wakati kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara
kutoka nje; kuongezeka kwa ulimbikizaji wa madai; Wafadhili kupendelea
zaidi kufadhili miradi moja kwa moja badala ya utaratibu wa kupitia
bajeti ya Serikali unaoiwezesha Serikali kupanga matumizi kulingana na
vipaumbele vyake: maandalizi ya miradi mingi kutokuwa kamili kuruhusu
hatua za utekelezaji kuanza katika muda uliopangwa; na mwenendo wa
kupungua kwa misaada na mikopo nafuu.
26. Mheshimiwa Spika, ili
kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuchukua hatua
zifuatazo: kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato;
kuimarisha mifumo na taasisi za udhibiti wa mapato na ulinzi wa
rasilimali za Taifa; kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kodi;
kuendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa walipa kodi kwenye
kanzidata ya walipa kodi; kuhuisha mifumo ya kielektroniki ya kumtambua
mlipa kodi; kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi hasa
yale yanayotokana na michango ya mashirika na wakala za Serikali;
kuzitaka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia
mifumo ya kielektroniki katika kukusanya maduhuli; na kutekeleza
makubaliano kati Serikali na Washirika wa Maendeleo juu ya mfumo
ulioboreshwa wa ushirikiano utakaoanza kutumika mwaka 2018/19. Hatua
nyingine ni pamoja na: kuimarisha benki za maendeleo ili zichangie
katika upatikanaji wa rasilimali fedha, hususan mikopo ya kibiashara ya
muda mrefu; kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara kwa ajili ya
kuchochea ushiriki wa Sekta Binafsi; kutoa mafunzo kwa wataalam wa
Wizara, Idara Zinazojitegemea na Taasisi za Serikali juu ya uandaaji wa
miradi ya maendeleo; kupitia Sheria ya uwekezaji kwa ubia (PPP); na
uandaaji wa Mkakati wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango wa
Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
SHABAHA NA MALENGO YA UCHUMI JUMLA 2018/19 – 2020/21
27.
Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha
muda wa kati (2018/19 – 2020/21) ni kama ifuatavyo:-
i. Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2018 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 7.0 mwaka 2017;
ii. Kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei kutoka wastani wa asilimia 5.3 Juni 2017 hadi asilimia 5.0 ifikapo Juni 2018;
iii. Mapato ya kodi kuwa asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 sawa na ilivyokuwa mwaka 2017/18;
iv.
Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 24.5 ya Pato la Taifa
mwaka 2018/19 ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka 2017/18;
v. Kupunguza nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kutoka asilimia 3.8 mwaka 2017/18 hadi asilimia 2.5 mwaka 2018/19; na
vi.
Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi
minne.
MISINGI YA MPANGO NA BAJETI (ASSUMPTIONS)
28. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha muda wa kati (2018/19 – 2020/21), misingi ya mpango na bajeti ni pamoja na:
i. Kuendelea kuimarishwa na kudumishwa kwa amani, usalama, utulivu na umoja nchini na nchi jirani;
ii.
Kuimarika kwa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kama vile Pato la Taifa, ukusanyaji wa mapato ya ndani na
mfumuko wa bei;
iii. Kuendelea kuimarika na kutengemaa kwa uchumi wa dunia;
iv. Kuendela kuwa na utulivu wa bei za mafuta katika soko la dunia; na
v. Kuwa na hali ya hewa nzuri ndani ya nchi na katika nchi jirani.
MAOTEO YA AWALI YA UKOMO WA BAJETI 2018/19
29.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi
na sera za bajeti kwa mwaka 2018/19, maoteo ya awali yanaonesha kuwa
jumla ya Shilingi bilioni 32,476 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika
katika kipindi hicho. Maoteo haya yatathibitishwa baada ya kufanya
uchambuzi wa mwenendo wa utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha nusu
ya kwanza ya mwaka 2017/18. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Shilingi
bilioni 22,088.2, sawa na asilimia 68 ya mahitaji yote. Kati ya hayo,
maoteo ya mapato ya kodi yatakuwa Shilingi bilioni 18,817.0 sawa na
asilimia 85.2 ya mapato ya ndani. Vile vile, mapato yasiyo ya kodi
yatakuwa Shilingi bilioni 2,423.5 na mapato kutoka vyanzo vya
Halmashauri yatakuwa Shilingi bilioni 847.7. Serikali inategemea kukopa
kiasi cha dola za Marekani milioni 600 sawa na Shilingi bilioni 1,374.0
kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na Shilingi bilioni
4,028.6 ni mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana
za Serikali zinazoiva.
Aidha, Shilingi bilioni 1,327 sawa na
asilimia 1 ya Pato la Taifa, itakuwa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili
ya kugharamia miradi ya maendeleo.
30. Mheshimiwa Spika,
katika maoteo hayo, Washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia
Shilingi bilioni 3,658.2 ambapo Shilingi bilioni 946.0 ni misaada na
mikopo nafuu ya kibajeti, Shilingi bilioni 2,153.3 ni misaada na mikopo
kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Shilingi bilioni 558.9 ni misaada na
mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.
31.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, Serikali itatumia jumla ya
Shilingi bilioni 32,476.0 ambapo matumizi ya kawaida ni Shilingi bilioni
20,227.6 na maendeleo ni Shilingi bilioni 12,248.3. Kati ya fedha za
matumizi ya kawaida, Shilingi bilioni 7,627.7 ni kwa ajili ya mishahara
ya watumishi wa Serikali na Taasisi za Umma na Shilingi bilioni 9,705.2
kwa ajili ya Deni la Taifa. Aidha, kwa upande wa matumizi ya maendeleo
kiasi cha Shilingi bilioni 9,536.2 au asilimia 76.6 ni fedha za ndani.
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2018/19
32.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka
2018/19 ni mwongozo katika uandaaji wa miradi na programu za maendeleo
itakayojumuishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2018/19 na
kitabu cha bajeti ya Maendeleo 2018/19 nitakavyowasilisha mwezi Juni
hapa Bungeni. Hivyo, ni matarajio ya Serikali kuwa Waheshimiwa Wabunge
watatumia fursa hii kutoa maoni yao yatakayojumuishwa katika Mpango wa
Maendeleo wa Taifa mwaka 2018/19.
33. Mheshimiwa Spika,
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu katika
mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano. Mapendekezo haya yamezingatia malengo ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21, hususan:- (a)
Kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi; (b) Kuimarisha kasi ya utekelezaji
wa Mpango, hasa kwa kutanzua changamoto za upatikanaji wa fedha
na
mitaji, upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji, na kuimarisha
mipango miji na maendeleo ya makazi; (c) Kuongeza uzalishaji wa bidhaa
za viwandani; (d) Kuongeza uwezo wa kupambana na umaskini; (e)
Kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii kwa kutoa huduma bora za afya,
elimu, maji na kinga kwa jamii; (f) Kuongeza matumizi ya teknolojia,
ubunifu, ujuzi na utoshelevu wa mahitaji ya rasilimali watu yenye weledi
unaohitajika kwa ustawi wa uchumi wa viwanda; na (g) kuhakikisha
usalama wa chakula na mahitaji ya lishe bora nchini.
Vipaumbele vya Mpango na Miradi Itakayopewa Msukumo wa Kipekee Mwaka 2018/19
34.
Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2018/19
vitazingatia maeneo manne ya kipaumbele ya Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Taifa wa Miaka Mitano. Aidha, maeneo hayo yamejumuisha miradi ya
kielelezo ambayo utekelezaji wake utapewa msukumo wa kipekee:-
(i) Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda:
Lengo
ni kuendelea kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana
nchini, hususan za kilimo, madini na gesi asilia. Katika eneo hili,
miradi itakayopewa msukumo wa kipekee ni pamoja na: Mradi wa Makaa ya
Mawe Mchuchuma; Kiwanda cha Kufua Chuma cha Liganga; Shamba la Miwa na
Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Ujenzi wa mtambo wa kusindika Gesi
Kimiminika; uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; na Kituo cha
Viwanda Kurasini. Aidha, Serikali itaendelea kupanua na kuimarisha
shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO ili kulifanya kuwa chombo
cha kuleta mageuzi ya viwanda nchini.
(ii) Kufungamanisha Uchumi na Maendeleo Watu:
Eneo
hili linalenga kuendeleza mafanikio ya ustawi wa maisha ya watanzania
hasa wa vijijini. Msukumo utakuwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma
za afya hususan huduma za kibingwa, elimu na ujuzi, huduma za ustawi wa
jamii; upatikanaji wa uhakika wa chakula na lishe bora; kuendelea
kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na
salama vijijini
na mijini; kusimamia rasilimali za maji nchini; na kuimarisha usimamizi
wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi. Aidha, Serikali itaendelea
kuimarisha usimamizi wa utawala bora ikiwa pamoja na kukamilisha azma ya
kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma.
(iii) Ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji:
Eneo
hili linalenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu,
ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, barabara,
madaraja na bandari), usafiri wa anga (viwanja vya ndege) na usafiri wa
majini (meli na vivuko). Miradi itakayopewa msukumo wa kipekee katika
eneo hili ni pamoja na: ujenzi wa bwawa na mitambo ya kufua umeme wa
Stiegler’s Gorge; ujenzi wa Reli ya Kati; na kuboresha Shirika la Ndege
Tanzania. Vile vile, Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa ugawaji na
usimamizi wa ardhi; kuboresha mazingira ya kibiashara ili kuvutia
uwekezaji na kupanua masoko; na kuendeleza ushirikiano wa kikanda na
kimataifa hususan kwa njia ya diplomasia ya kiuchumi.
(iv)
Kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Mpango: hatua zinazopendekezwa
zinalenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za
utekelezaji wa Mpango, ikiwa ni pamoja na: kuimarisha mifumo na taasisi
za utekelezaji wa Mpango; kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa
uhakika wa rasilimali fedha kwa maandalizi na utekelezaji wa miradi; na
kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
Miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
35.
Mheshimiwa Spika, Mpango umebainisha miradi mikubwa ya maendeleo
inayotarajiwa kutekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na
Binafsi. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa mabasi yaendayo
haraka Dar es Salaam; kiwanda cha kuzalisha madawa muhimu na vifaa tiba;
na mradi wa Dar es Salaam – Chalinze Toll Road. Msukumo utawekwa
kuongeza idadi ya miradi itakayotekelezwa kwa mfumo wa PPP.
Mikakati ya Kushirikisha Sekta Binafsi kwa mwaka 2018/19
36.
Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi ndio mtekelezaji mkuu wa Mpango kadri
ya dhana ya kujenga uchumi wa viwanda. Serikali imeweka mikakati
inayolenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa
mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mikakati ya kubainisha maeneo
yatakayowezesha kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuainisha vivutio
kwa wawekezaji katika maeneo ya kipaumbele; kuboresha zaidi mfumo rekebu
na jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi kuhusu
uwekezaji (investors round-table); kufanya mapitio ya sheria ya
uwekezaji wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi; kuendeleza
maboresho ya kimifumo na kitaasisi kuhusiana na ufumbuzi wa mahitaji ya
sekta binafsi. Aidha, Serikali itaendelea kuziimarisha benki za ndani za
maendeleo ili ziweze kukidhi ongezeko la mahitaji ya mikopo na udhamini
kwa sekta binafsi.
MAELEKEZO MAHSUSI KATIKA UANDAAJI WA MIPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2018/19
37.
Mheshimiwa Spika, Maafisa Masuuli wanatakiwa kuzingatia Sheria ya
Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuunda
Kamati za Mipango na Bajeti na kuhakikisha Kamati hizo zinatekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 17(3) cha Kanuni za Bajeti za
mwaka 2015. Masuala muhimu ambayo Maafisa Masuuli wote wanapaswa
kuzingatia wakati wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti kama ifuatavyo:
Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani
38.
Mheshimiwa Spika, Maafisa masuuli wanaelekezwa: kuhakikisha kuwa
makusanyo yote yanawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali; kuendelea
kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato; kuhakikisha zabuni za watoa
huduma na makandarasi zinatolewa kwa wanaotumia mashine za
kielektroniki; kukusanya mapato kutoka vyanzo bunifu vilivyoainishwa
katika Mkakati wa Ugharamiaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano pamoja na vyanzo vingine; kutoingia mikataba yenye vifungu
vya sheria vinavyohusiana na misamaha ya kodi bila kupata ridhaa ya
Waziri wa Fedha na Mipango; na
kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kutoa gawio stahiki kwa Serikali.
Kudhibiti Matumizi na Kupunguza Gharama
39.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Serikali inadhibiti na kupunguza
gharama za uendeshaji, Wizara, Idara Zinazojitegema, Wakala, Taasisi za
Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinaelekezwa: kuendelea kufanya uhakiki wa watumishi ili kuhakikisha
kuwa mishahara inalipwa kwa watumishi wanaostahili; kuendelea kupunguza
matumizi ya Serikali kwa kutumia Taasisi za Serikali zenye gharama nafuu
na huduma bora; kuhakikisha kuwa mikataba yote inayoingiwa na Serikali
na Taasisi zake inakuwa katika Shilingi ya Tanzania isipokuwa kwa
mikataba inayohusisha biashara za kimataifa; kufanya tathmini ya gharama
za uendeshaji wa Taasisi za Serikali ili kuchukua hatua stahiki; na
kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara zinapata
faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Kulipa na Kuzuia Ongezeko la Madeni ya Serikali
40.
Mheshimiwa Spika, katika kulipa na kudhibiti ongezeko la madeni ya
Serikali, Maafisa Masuuli wanaagizwa: kuhakikisha madai yote
yamehakikiwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali na kuingizwa kwenye
hesabu za Fungu husika (Financial Statement); kutenga fedha za kulipa
madeni yaliyohakikiwa; kutekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa na
Serikali kuhusu ununuzi wa bidhaa na huduma; kutoingia mikataba ya
miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha; na kuzingatia
matumizi ya Hati ya ununuzi (LPO) zinazotolewa kwenye Mfumo wa Malipo
(IFMS) ili kudhibiti ulimbikizaji wa madai.
Maelekezo Mengine
41.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelekezo hayo mahsusi, Maafisa Masuuli pia
wanaelekezwa: kutoa taarifa za utekelezaji kwa kuzingatia muundo wa
utoaji taarifa uliobainishwa katika Mwongozo; kuhakikisha mipango na
bajeti inawekewa viashiria, vigezo na shabaha bayana ambavyo usimamizi
wa utekelezaji utavizingatia; na kutekeleza Sera ya Ugatuaji wa Madaraka
kwa
kuhakikisha kuwa fedha zinatengwa kwenye Halmashauri husika badala ya kutengwa kwenye bajeti za Wizara.
HITIMISHO
42.
Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka
2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19
yaliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu yanalenga kujenga uelewa
wa pamoja juu ya: hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti na miradi ya
maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopita; maeneo ya kiupaumbele na bajeti
yanayopendekezwa kwa mwaka 2018/19 katika kukuza uchumi na kupunguza
umaskini; hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na Serikali katika kuvutia
uwekezaji wa sekta binafsi hususan katika sekta ya viwanda; na kwamba
juhudi za makusudi zinahitajika katika kufikia malengo ya Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2025 ya kujenga uchumi wenye hadhi ya kipato cha
kati. Msukumo mkubwa wa Serikali utawekwa katika mikakati ya kuongeza
mapato, kupunguza gharama na matumizi ya uendeshaji wa Serikali na
kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.
43. Mheshimiwa Spika,
Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Mashirika na Taasisi za Umma zinaelekezwa
kuzingatia Mwongozo katika kuandaa mipango na bajeti zao. Vile vile,
zinaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19.
44.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda kutoa
shukurani za dhati kwa wadau na wananchi wote kwa juhudi wanazoendelea
kufanya katika utekelezaji wa mipango na bajeti. Natoa rai kwa Sekta
Binafsi na wananchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
hususan katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza na kutekeleza
wajibu wa kulipa kodi.
45. Mheshimiwa Spika, hotuba hii
pamoja na vitabu vya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka
2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19
vitapatikana pia katika tovuti za Wizara ya Fedha na Mipango
(www.mof.go.tz na www.mipango.go.tz).
46. Mheshimiwa Spika, baada
ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili, kutoa
maoni na kuishauri Serikali kuhusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na
Bajeti ya Mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2018/19.
47. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
0 comments:
Post a Comment