SERIKALI jana imewasilisha ukomo wa bajeti na mpango wa maendeleo wa
miaka mitano unaolenga kuiweka Tanzania katika safari kamili ya viwanda.
Aidha serikali inatarajia kutumia kiasi cha Sh trilioni 32.476 kwa
mwaka 2018/19 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.4 ya bajeti ya
mwaka 2017/18 ambazo zilikuwa Sh trilioni 31.712.
Aidha, imetaja shabaha na malengo ya uchumi sita ambayo ni pamoja na
kuhakikisha ukuaji wa Pato Halisi la Taifa, kudhibiti kasi ya mfumuko wa
bei na kukua kwa mapato ya kodi. Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 22.088
sawa na asilimia 68 ya mahitaji yote, ni mapato ya ndani ambayo mapato
ya kodi ni Sh trilioni 18.8 sawa na asilimia 85.2 ya mapato yote, mapato
yasiyo ya kodi ni Sh tril 2.4.
Mapato ya halmashauri ni Sh bilioni 847.7 na hivyo ili kukamilisha
bajeti serikali inahitaji Sh trilioni 10.388 ambazo ni mikopo kutoka
ndani na nje ya nchi. Kiasi hicho cha fedha kilitajwa na Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni jana
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na
Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19.
Akitoa ufafanuzi kuhusu makisio ya bajeti hiyo ya mwaka 2018/19 ya Sh
trilioni 32.476, Dk Mpango alisema kati yake Sh trilioni 20.227
zitakuwa za matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.248 ni za maendeleo.
Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh trilioni 7.627 ni kwa ajili
ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma, Sh trilioni
9.705 ni kwa ajili ya deni la taifa ambalo hadi Juni mwaka huu lilikua
na kufikia dola za Marekani milioni 26,115.2 sawa na ongezeko la
asilimia 17 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 22,320.76, katika
kipindi hicho mwaka 2016.
Alisema kwa upande wa fedha za matumizi ya maendeleo, Sh trilioni
9.536 au asilimia 76.6 ni fedha za ndani na zinazobaki zitakopwa kutoka
vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Dk Mpango alitaja shabaha na malengo ya uchumi sita katika
kipindi cha muda wa kati cha mwaka 2018/19 hadi mwaka 2020/21 kuwa ni
kuhakikisha kwamba ukuaji wa pato la halisi ya Taifa unafikia asilimia
7.1 katika mwaka 2017.
“Pia shabaha na malengo ya uchumi yanalenga kudhibiti kasi ya mfumo
wa bei kutoka wastani wa asilimia 5.3 ya mwezi Juni mwaka huu hadi
asilimia 5.0 ifikapo Juni mwakani,” alisema.
Alisema mapato ya kodi kukua na kuwa asilimia 14.2 ya Pato la Taifa
katika mwaka 2018/19 sawa na ilivyokuwa katika mwaka 2017/18. Dk Mpango
alisema matumizi ya serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 24.5 ya Pato la
Taifa katika mwaka 2018/19 ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka
2017/18.
“Kupunguza nakisi ya bajeti ikijumuishwa na misaada kutoka asilimia
3.8 mwaka 2017/18 hadi asilimia 2.5 mwaka 2018/19,” alisema Dk Mpango.
Pia alisema kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi
mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi
kisichopungua miezi minne.
Dk Mpango alisema misingi ya mpango na bajeti mitano katika kipindi
hicho ni pamoja na kuendelea kuimarishwa na kudumishwa kwa amani,
usalama, utulivu na umoja nchini na nchi jirani.
“Kuimarisha kwa viashiria va uchumi na maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kama vile Pato la Taifa, ukusanyaji wa mapato ya ndani na
mfumuko wa bei,” alisema. Pia alisema ni kuendelea kuimarika na
kutengemaa kwa uchumi wa dunia, kuendelea kuwa na utulivu wa bei za
mafuta katika soko la dunia na kuwa na hali ya hewa nzuri ndani ya nchi
katika nchi jirani.
Alisema mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu
katika mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa
miaka mitano. Alisema mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo yamezingatia
Malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka mitano
(2016/17-2020/21) hususani katika kuendeleza kasi ya ukuaji uchumi na
kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mpango hasa kwa kutatua changamoto za
upatikanaji wa fedha na mitaji.
“Pia yamezingatia upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji na
kuimarisha mipango miji na maendeleo ya makazi, kuongeza uzalishaji wa
bidhaa viwandani, kuongeza uwezo wa kupambana na umaskini na kuimarisha
ustawi na maendeleo ya jamii kwa kutoa huduma bora afya, elimu, maji na
kinga kwa jamii,” alisema.
Pia kuongeza matumizi ya teknolojia, ubunifu ujuzi na utoshelevu wa
mahitaji ya rasilimali watu wenye weledi unaohitaji kwa ustawi wa uchumi
wa viwanda na kuharakisha usalama wa chakula na majitaji ya lishe bora
nchini.
Waziri Mpango alivataja vipaumbele na miradi itakayopewa msukumo wa
kipekee katika mwaka 2018/19 ambayo itakuwa katika maeneo manne
yanayohusu Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano.
Alisema miradi kielelezo ambayo utekelezaji wake utapewa msuko wa
kipekee katika kujenga viwanda vya kukuza uchumi na hasa katika ujenzi
wa msingi wa uchumi wa viwanda ni pamoja na mradi wa makaa ya mawe
Mchuchuma, Kiwanda cha kufua chuma cha Liganga, shamba la miwa na
kiwanda cha sukari Mkulazi, ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi
kimiminika Lindi, uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi na kituo cha
viwanda cha Kurasini.
Msukumo mwingine upo katika kufungamanisha uchumi na maendeleo ya
watu eneo hili linalenga kuendeleza mafanikio ya ustawi wa maisha ya
Watanzania hasa vijiji kwa kuboresha huduma za afya hasa za kibingwa,
elimu na ujuzi huduma za ustawi wa jamii na upatikanaji wa uhakika wa
chakula na lishe bora.
Dk Mpango alisema msukumo mwingine upo katika ujenzi wa mazingira
wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji eneo ambalo linalenga
kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya nishati, usafirishaji,
usafiri wa anga na usafiri wa majini.
“Miradi itakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi wa bwawa na mitambo
ya kufua umeme Stiegler’s Gorge, ujenzi wa reli ya kati na kuboresha
Shirika la Ndege Tanzania,” alisema.
Dk Mpango alisema msukumo upo katika kuimarisha usimamizi na
utekelezaji wa mipango ambako kunalenga ufuatiliaji, tathmini na utoaji
wa taarifa za utekelezaji wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha
mifumo na taasisi za utekelezaji wa mpango, kuweka mfumo utakaowezesha
upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha kwa maandalizi ya utekelezaji
wa miradi na kuweka vigezo vya upimaji mafanikio na utekelezaji.
“Serikali inaweza mkazo katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma
na binafsi, miongoni mwa miradi hiyo ni wa mabasi yaendayo haraka Dar es
Salaam, kiwanda za kuzalisha dawa muhimu na vifaa tiba, na mradi wa Dar
es Salaam-Chalinze na itaendelea kuongeza idadi ya miradi hiyo iliyo
katika mfumo wa PPP,” alisema.
Dk Mpango alisema serikali imeweka mkakati wa kushirikisha sekta
binafsi katima mwaka 2018/19, kwani sekta binafsi ndio mtekelezaji mkuu
wa mpango kadiri ya dhana ya kujenga uchumi wa viswanda.
“Serikali imeweka mikakati inayolenga kuimarisha ushiriki wa sekta
binafsi katika utekelezaji wa mpango, ikiwa ni pamoja na kuimarisha
mikakati ya kubainisha maeneo yatakayowezesha kuvutia wawekezaji wa
sektsa binafsi na kuainisha vivuto kwa wawekezaji,” alisema.
Mpango alitoa maelekezo mahsusi katika uandaaji wa mipango na bajeti
kwa mwaka 2018/19 kwa mujibu wa kifungu cha 17 (3) kanuni ya bajeti ya
mwaka 2015, ambao inawataka maofisa masuhuli kuzingatia, ikiwa ni pamoja
na ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 unalenga
kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hali ya uchumi, utekelezaji wa bajeti
na miradi ya maendeleo kwa mwaka uliopita na hatua mbalimbali
zinazochukuliwa na serikali katika kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi
katika viwanda na juhudi za kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya
Taifa 2025 ya kujenga uchumi wenye hadhi ya kipato cha kati.CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment