UKAMILISHAJI wa Mchakato wa Katiba Mpya si kipaumbele cha serikali
bali inataka kwanza kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za jamii kama
elimu, afya, maji na miundombinu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa tamko hilo jana wakati akijibu
swali la Mbunge wa Temeke, Abdallah Ali Mtolea (CUF) aliyetaka kujua
lini serikali itakamilisha mchakato wa katiba ulioanzishwa na ile ya
awamu ya nne.
Waziri Mkuu alisema, suala la Katiba si miongoni mwa vipaumbele vya
Serikali ya Awamu ya Tano, kwani kukamilisha kunahitaji fedha nyingi na
ni gharama kubwa na kwa sasa fedha zinazokusanywa zinaekelezwa katika
kuboresha huduma za afya, elimu na maji.
Majaliwa alisema kila mwaka serikali inaweka vipaumbele vyake, kwa
sasa vipaumbele vya serikali ni kuwapa wananchi huduma za jamii. Alisema
mchakato wa Katiba unalenga kufanya marekebisho ya mambo mbalimbali
ambayo yamo katika katiba ya sasa, hivyo hiyo iliyopo inaweza kuendelea
kutumika hadi hapo fedha zitakapopatikana kwa ajili ya mchakato huo na
pale itakapokuwa kipaumbele cha serikali.
“Mchakato wa Katiba ni gharama na serikali inatambua umuhimu wake,
hivyo kwa sasa inalenga kuboresha huduma za wananchi kwa kutumia katiba
iliyopo,” alisema Majaliwa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment