Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma
MBUNGE wa Geita Vijijini, Joseph Kisheku ‘Musukuma’ (CCM) amewapinga
wabunge wanaotoka mikoa inayolima mahindi waliokuwa wanaitaka serikali
kuruhusu mahindi kuuzwa nje ya nchi, akisema mahindi yaliyokosa soko si
ya wakulima masikini hivyo serikali ishikilie msimamo wake wa kuzuia
mazao hayo kuuzwa.
Awali wabunge waliochangia suala la mahindi, walidai mahindi yamekosa
soko nchini na wakulima wamebaki majumbani na mahindi yao hivyo
wanaiomba Serikali iwaruhusu wauze nje ya nchi kupata fedha kujikimu na
kulima tena.
Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Mbunge wa Manyoni Mashariki
Daniel Mtupa (CCM) alisema kutokana na Serikali kuzuia mahindi kuuzwa
nje ya nchi na kushindwa kununua, uchumi wa wananchi umeyumba.
Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy (CCM) alisema kutokana na wakulima
kushindwa kuuza mahindi yao, mwaka huu hawataweza kulima kutokana na
kukosa fedha za mbolea na mbegu hivyo kuna uwezekano mkubwa kukatokea
njaa.
“Mbona nyinyi mishahara yenu mnatumia mtakavyo, mnaongeza wake na
kunywea pombe kwa nini mkulima mnampangia masharti, mnaona wivu akiuza
mahindi akaweka bati kwenye nyumba yake,” alihoji Kessy.
Pia mbunge wa Lupembe, Joram Hongori (CCM) alisema wakulima wa
mahindi wameuza gunia moja kati ya Sh 20,000 na 25,000 na bei hiyo ndogo
imetokana na kukosa soko baada ya serikali kuwazuia kuuza nje ya nchi
wakati Wakala wa NFRA imenunua mahindi kidogo.
“Kutokana na kuuza kwa bei ndogo, wakulima wamekosa pesa za mbolea
hivyo katika msimu ujao wengi watashindwa kulima. Tunaiomba serikali
iangalie kuondoa katazo lao na ifungue mipaka waweze kuuza kwa bei nzuri
nje ya nchi ili watoto wao waende shule,” alisema.
Naye Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) alisema, “Sio wakulima
wote wanalima kwa ajili ya chakula bali wengine hulima kwa biashara.
Mfano Sumry ameacha biashara ya mabasi na amelima ekari 1,000 za mahindi
lakini unamzuia kuuza mahindi yake. Serikali ioneshe nia ya dhati
kusaidia kilimo,” alisema.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment