Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma
WABUNGE wamelaani baadhi ya wabunge wenzao kujadili hoja kwa ukanda
na kutaka wachuje maneno kabla ya kusema bungeni huku wakimtaka Spika
Job Ndugai awaadhibu.
Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM) aliyeingia bungeni humo tangu
mwaka 1995, alionesha kukerwa na ukanda kujadiliwa ndani ya Bunge tangu
mkutano huu wa tisa uanze.
Alisema kitendo cha kufananisha maendeleo anayoleta Rais John
Magufuli kuwa anapendelea Kanda ya Ziwa si kauli nzuri. “Jana watu
(wabunge) humu walitokwa mapovu kwa ukanda, sisi wabunge tuchuje maneno
yetu kabla ya kuyatoa. Sasa Bunge linajadili ukanda tukitoka huko
tutakuja kujadili ukabila, rangi na dini zetu.
Tusiwagawe wananchi kwa ukanda,” Ndassa alisema. …Tuungane kupigana
vita ya uchumi, tuna maadui wengi, tumuunge mkono Rais kwenye vita hii
ya uchumi. Spika naomba akisimama mbunge kuzungumzia ukanda una mamlaka
ya kumshughulikia,” alisema mbunge huyo.
Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM) alitaka mbunge
anayezungumzia ukanda azuiwe kwani anakwenda kinyume na Katiba ya nchi
inayozuia ubaguzi na kugawa Watanzania. “Sijaridhika na mjadala wa
ukanda, asiyeona kazi nzuri ya Rais Magufuli ni mgonjwa, analinda
rasilimali za nchi, asipingwe,” alisema.
Hata hivyo, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe ambaye ni Kiongozi wa
upinzani bungeni na ambaye wabunge wa chama chake tangu Bunge lianze
wamekuwa wakimlaumu Rais Magufuli anapeleka maendeleo na kufanya ziara
Kanda ya Ziwa na kutokwenda mikoa mingine naye alikiri kuzungumzia
ukanda bungeni si jambo zuri.
“Nakubaliana na Ndassa kuzungumzia ukanda si vizuri lakini aangalie
chanzo ni nini. Mbona miaka minne iliyopita hatujazungumza sasa kuna
mambo yanafanyika si sawa na msiba utatuumbua,” alisema Mbowe.
Ukiacha ukanda, Mbunge Ndassa alimlaumu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dk Philip Mpango akidai ana kiburi, hasikilizi ushauri wa wabunge hasa
wa Kamati ya Bajeti na kusisitiza “Dk Mpango una ka arrogance fulani,
wabunge wa CCM wanakuheshimu, lakini huisaidii Serikali na hata kukupata
ni ngumu, simu za wabunge hupokei jitahidi kusikiliza ushauri.
Ipo siku mtakwama na wataalamu wenzako na mtatuomba tuwakwamue nasi
tutasema hapana, wewe si msikivu kwa wabunge, badilika, sisi sote tupo
hapa katika boti moja,” alimweleza.
Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) alimlaumu Dk Mpango kuwa
hasikilizi ushauri wa Kamati ya Bajeti na atamharibia Rais Magufuli
mwaka 2020 huku akifafanua: Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba
(CCM) alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/2019
unaojadiliwa bungeni hauna tofauti na wa mwaka jana na mwaka juzi na
unazungumzia kukusanya kodi bila kuongeza uzalishaji na haushirikishi
sekta binafsi.
Spika Ndugai aliwataka wabunge wa CCM kufunguka mambo ya msingi
katika kujadilli mpango huo ili kumsaidia Waziri Mpango kutokuwa na
mpango mbovu wa maendeleo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment