KATIKA kuelekea katika Tanzania ya viwanda, Spika wa Bunge, Job
Ndugai amewataka Watanzania wazalendo kuwekeza miradi mbalimbali hapa
nchini badala ya kusubiri watu kutoka mataifa ya nje.
Ndugai alisema kumekuwepo na kasumba ya Watanzania kufanyiana hiana
wao kwa wao pale inapotokea mwekezaji mzawa amewekeza mradi mkubwa na
kuanza kuzushiwa kuwa ni mwizi na fisadi. Alisema anashangazwa na tabia
ya baadhi ya wananchi kuwashabikia wawekezaji kutoka nje huku wazawa
wakizushiwa mambo badala ya kutiana moyo, jambo ambalo alisema siyo la
kizalendo.
Ndugai alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Hoteli ya Fantasy
Village iliyopo Msalato Senje ambayo inamilikiwa na Mussa Hassan Musa
ambayo itagharimu Sh bilioni nne hadi kukamilika kwake.
Alisema si kila Mtanzania anayewekeza kwa mradi mkubwa ni mwizi na
fisadi bali anawekeza fedha zake nchini. “Hili limekuwa likinivunja
nguvu, unashangaa watu wanawasifia wawekezaji kutoka China, Uarabuni,
India pamoja na nchi nyingine, lakini ikitoa mwekezaji kutoka hapa
utasikia wanaanza kumzushia kuwa ni fisadi, mwizi hapo unajiuliza hivi
ni kweli kila mwekezaji wa ndani ni mwizi au fisadi,” alihoji Spika.
Mussa ambaye ni mwekezaji wa ndani, alisema pamoja na kuwa amewekeza
katika eneo la Msalato, atahakikisha anajihusisha na maendeleo ya jamii
inayomzunguka kwa lengo kuinua jamii kwa ujumla.
Alisema mradi wake aliowekeza unatarajiwa kutoa ajira ya watumishi
700 kwa ngazi mbalimbali huku walio wengi wakiwa Watanzania hususani
kutoka mkoa wa Dodoma na maeneo mbalimbali ya Tanzania. Hata hivyo,
alisema hatua ya kwanza atawekeza zaidi katika sekta ya afya kulingana
na mahitaji halisi ya wananchi wa maeneo ya Msalato na ataendelea
kuhakikisha shughuli za kimaendeleo zinapatikana.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment