SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema wabunge wanatakiwa kupigwa msasa
katika suala la maadili kutokana na wananchi wengi kulalamika kuhusu
maadili yao, huku akimuomba Kamishna wa Maadili, kuangalia uwezekano wa
watunga sheria hao kula kiapo cha uadilifu kama ilivyo kwa watumishi wa
umma.
Aidha, wabunge kwa upande wao, wamekuwa na maoni tofauti kuhusu suala
hilo la maadili baadhi yao wakihoji manufaa ya kujaza fomu za maadili
kila mwaka, lakini hawaoni hatua zikichukuliwa kwa wanaokiuka sheria
hiyo, na wengine wakihojiwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa
uadilifu kupandishwa vyeo.
Spika Ndugai na wabunge hao walizungumza hayo jana mjini hapa wakati
wa semina ya maadili na udhibiti wa rushwa kwa wabunge iliyoandaliwa na
Mtandao wa Wabunge Wanaopambana na Rushwa (APNAC) kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Spika Ndugai alisema
wabunge wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wamekuwa hawana maadili hivyo
akaomba wabunge wapigwe msasa katika eneo hilo.
“Tutakubaliana na waheshimiwa wabunge katika eneo ambalo tunatakiwa
kupigwa brashi ni katika eneo la maadili kwani tumenukuliwa na vyombo
vya habari na wananchi wametulalamikia kwamba baadhi hatuna maadili,”
alisema Spika Ndugai. Alimuomba Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold
Nsekela kuangalia uwezekano wa wabunge kula kiapo cha maadili pindi
wanapoapishwa.
“Waheshimiwa wabunge tunapoapishana bado hatuna kiapo, napenda
kushauri kama kuna umuhimu hili liwepo. Tunapaswa kujua ni namna gani
tunaishi katika jamii, maadili yatusaidie katika uongozi wetu,”
aliongeza Spika Ndugai. Katika mchango wake, Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy
(CCM) alihoji kuwa wamekuwa wakijaza fomu za maadili, lakini hakuna
hatua zozote zilizochukuliwa kwa wanaokiuka. “Baadhi ya viongozi
walikula pesa na wakarudisha sasa hawa ninyi viongozi wa Maadili
mmechukua hatua gani kwa hao viongozi nashangaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema nyinyi mnasimamia maadili ya viongozi
na kila mwaka mnajaza fomu, na viongozi wa nchi hii wana majengo ya
ajabu na wanajaza uongo. Mfano, EPA wengine wamerudisha fedha wengine
hawajarejesha, wanatanua tu na wengine wapo ndani kwa ushahidi,”
alieleza mbunge huyo machachari. “Sasa ninyi kama viongozi mnachukua
hatua gani kwa hawa watu ambao wana majumba hayalingani na mishahara yao
kila siku tunajaza tu fomu.
Mimi ni mbunge miaka saba kila mwaka najaza tu fomu sioni hatua
zozote, mimi nalikataa hili.” Wabunge wengine wakiwamo wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walitaka kupata ufafanuzi kutoka kwa
Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Nsekela ni kwa nini baadhi ya viongozi
wakiwemo wakuu wa wilaya wanaokiuka kanuni za maadili, lakini wamekuwa
wakipandishwa vyeo.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema) alihoji, “Kama
Mwenyekiti wa Maadili hapa katikati kulitokea purukushani nyingi tu,
lakini wengine tulikuwa hatuamini, lakini huyo aliyekuwa akituhumiwa kwa
rushwa ambaye ni kiongozi katika serikali amesema hadharani na kwenye
vyombo vya habari nadhani hata wewe unajua kwa sababu imezunguka sana.
Hamuoni kama tunadanganyana katika mambo ambayo yana uhalisia.” Kwa
upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) alisema:
“Tunaomba sana wewe Mheshimiwa Jaji siyo nyie mnaangalia maadili kwa
watu wadogo wadogo muangalie na kwa hawa watu wakubwa ambao wanafanya
mambo ili baadaye waweze kupandishwa vyeo zaidi kuliko Watanzania
wanavyotarajia.”
Akijibu hoja hizo, Jaji mstaafu Nsekela alisema maswali aliyoulizwa
siyo ya maadili na angependa ulizwe masuala yanahusu maadili. “Jambo la
kwanza lazima uangalie sheria inasemaje. Waheshimiwa wabunge
tunapozungumzia maadili ni lazima mpate sheria mliyoitunga inasema nini,
nadhani kwa hilo nimeeleweka.
Hata alilouliza Ally Kessy alihoji waliorudisha fedha sijui ni kina
nani hao ila tuje kwenye jambo la msingi hilo jambo lipo katika Sheria
ya Maadili na sisi tunashughulikia maadili siwezi kwenda katika jambo
alinihusu kwa hiyo wabunge mnielewe,” alifafanua.
“Maadili ninayoyazungumzia mimi ni ya sheria ya mwaka 1995 kama
ilivyorekebishwa mara mbili inawezekana kuna maovu yanatendeka, lakini
je hayo yapo katika sheria yangu. Maadili yanayozungumziwa ni yale
ambayo yapo katika sheria, mfano sheria ya rushwa hiyo haipo kwangu ndio
maana adhabu zangu ni kuteremshwa cheo, kujiuzulu.”
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment