SERIKALI imewaadhibu kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria,
watumishi 1,595 kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa
Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
baada ya kubainika ndiyo walisababisha kuajiri na kuajiriwa kwa
watumishi hewa nchini.
Aidha, Serikali imesema itaendelea kubuni na kutekeleza mikakati
kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa na watumishi sahihi, wenye elimu na
taaluma sahihi na wanafanya kazi mahali sahihi kuongeza ufanisi na
kuiwezesha Serikali kufikia azma yake ya kuwa na uchumi wa kati na wa
viwanda nchini.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro amesema hayo alipowasilisha taarifa ya
uhakiki wa watumishi na vyeti vya kufaulu mtihani wa kidato cha nne,
cha sita na ualimu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
Dodoma. Hata hivyo, Dk Ndumbaro aliyetoa taarifa hiyo mwisho mwa wiki
hakusema watumishi walichukuliwa hatua gani za kinidhamu kwa ushiriki
wao katika suala la kuajiri watumishi hewa zaidi ya 16,000.
Alisema ili kukabiliana na tatizo la watumishi wa umma kughushi vyeti
vya elimu na taaluma, Serikali na wadau wengine inabuni na kutekeleza
mikakati na hatua kubaini na kudhibiti vyeti vya kughushi nchini.
Alisema ili kudhibiti watumishi kujipatia ajira kwa vyeti vya
kughushi, Serikali imejipanga kuhakikisha vyeti vya taaluma na elimu vya
watumishi wapya na wanaorudi katika ajira kwa sababu mbalimbali za
kutoka likizo bila malipo, mikataba, uhamisho na ushikizwaji
vinahakikiwa na mamlaka husika kabla ya kuingizwa na kuidhinishwa kwenye
orodha ya malipo ya mishahara kuendelea na kazi walizokuwa nazo.
“Waajiri wote katika sekta ya umma wameelekezwa kutekeleza agizo hili
pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kuwa
na vyeti vya kughushi,” alieleza Dk Ndumbaro.
Ili kuwa na taarifa sahihi za watumishi nchini, alisema Serikali
imepanga kuunganisha na kuoanisha mifumo ya kimkakati ikiwemo ya taarifa
za watu (Mfumo wa HCMIS, NIDA, RITA, NECTA na TRA) kuongeza usahihi wa
taarifa za watumishi, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa
mbalimbali za mtumishi na kurahisisha ubadilishanaji na uhakiki wa
taarifa na nyaraka za watumishi wa umma.
Dk Ndumbaro alisema kwa kuanzia, uoanishaji wa taarifa za usajili za
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na zilizomo kwenye Mfumo wa
HCMIS unaendelea. Ndumbaro alisema Serikali ina mpango wa kupanua wigo
wa uhakiki wa vyeti kwa kuhakiki vyeti vya elimu ya juu na taaluma
kulingana na matakwa ya miundo ya maendeleo ya utumishi ya kila kada kwa
watumishi wasio wa kada za kisiasa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment