Home » » CCM Dodoma wampongeza Rais kuwasaidia watoto wenye Mahitaji Maalum

CCM Dodoma wampongeza Rais kuwasaidia watoto wenye Mahitaji Maalum


Kamati ya siasa mkoa wa Dodoma wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwasaidia wenye mahitaji maalum ikiwemo kuwajengea mabweni mawili kwa ajili yao katika Shule ya Msingi Iboni iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kondoa kata ya Chemchem.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Dodoma Ndg. Pili Agustino wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa mabweni mawili yaliyojengwa katika shule hiyo hivi karibuni.

“Nakumbuka nilikuja hapa mwaka 2023 tulikuja hapa tulikuwa bado hatujaanza ujenzi tukaongea na kupokea changamoto za hawa watoto ambapo wengine walikuwa wanatembea umbali mrefu na wazazi wao walikuwa wanashindwa kuwaleta hapa kutokana na changamoto ya kipato walizonazo,”amesema Katibu Pili

Ameendelea kueleza kuwa kutokana na kuwa Mheshimiwa Rais ni msikivu na anawapenda watoto akasikia kilio chao na akawaletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya watoto wenye mahitaji maalum ambapo wanasoma makika mazingira mazuri na salama na kuondokana na hali ya awali ambapo walikuwa wanasoma katika mazingira magumu.  

Aidha amewataka walimu kuyatunza mabweni hayo na kuhakikisha wanafunzi wanayatumia vizuri ili wenzao watakaokuja waweze kuyatumia yakiwa katika hali nzuri na imara kwani watoto hao ni wenye mahitaji maalum na wanatakiwa walelewe vizuri na kuelekezwa kufanya vitu mbalimbali.

“Tuna imani shule hii itaendelea kuwapokea na watoto wengine kutoka mikoa na wilaya nyingine si Kondoa tu hivyo tunawakaribisha wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kwani mabweni ni mazuri na salama na tuache tabia ya kuwaficha watoto ndani tuwalete shule kwani wanaweza kusoma na kufaulu vizuri na kupata kazi,”amesisitiza Katibu Pili

Akiongea kwa niaba ya wenzake mwanafunzi Rahma Ramadhani mwenye ulemavu wa macho amemshukuru Rais kwa kuwajengea mabweni na kumuombea ili apate fedha zaidi ambazo zitasaidia katika ununuzi wa vifaa vya kujifunzia shuleni hapo ambavyo vinakosekana shuleni hapo.

Akisoma awali taarifa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iboni Mwalimu Charles Phabian amesema shule hiyo ilipokea fedha shilingi milioni 142 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja, vitanda na magodoro pamoja na shilingi milioni 128 kutoka serikali kuu kwaajili ya ujenzi wa bweni na vitanda vya wanafunzi wenye mahitaji maalum ambayo yote yamekamilika.

Mabweni yaliyojengwa katika Shule ya Msingi Iboni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum yamekamilika ambapo Kamati ya Siasa mkoa imeshauri yaanze kutumika mapema mwezi Agosti na yatahudumia wanafunzi kutoka ndani nan je ya Kondoa na yana uwezo wa kubeba wanafunzi 200 wakike 120 na kiume 80 ambapo kwa sasa kuna jumla ya watoto 30 wenye mahitaji maalum kwenye shule hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Ndg. Said Majaliwa akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi katika Shule ya Msingi Iboni
Mkuu wa Shule ya Msingi Iboni Mwalimu Charles Phabian akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa mabweni mbele ya kamati ya siasa mkoa wa Dodoma
Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa wamejipanga na kusikiliza ujumbe kutoka kwa viongozi wa kamati ya siasa mkoa wa Dodoma baada ya kutembelea shuleni hapo.
Muonekano wa Bweni lawanafunzi wa kiume wenye mahitaji maalum lililojengwa katika Shule ya Msingi Iboni Kondoa Mji
Muonekano wa Bweni la wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalum  lililojengwa katika Shule ya Msingi Iboni  Kondoa Mji
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa