Home » » TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU




Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imetekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ya kuchagua na kuendesha mafunzo ya vinara wa ufuatiliaji na uthamini katika taasisi za umma.

Mmoja wa Waratibu wa mafunzo ya vinara yaliyotolewa na wawezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, hivi karibuni Bw. Elirehema Saiteru, Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa TANROADS amesema kuwa wameendesha mafunzo kwa watumishi kutoka Makao Makuu na mikoa yote 26 ya Tanzania, yaliyofanyika mkoani Morogoro, kulingana na mwongozo uliotolewa mwezi Juni 2024 jijini Dodoma.

Bw. Saiteru amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa mwongozo wa kuchaguliwa kwa vinara watakaokuwa wakifanya ufuatiliaji na tathimini ya miradi iliyopo chini ya taasisi hii.

“Baada ya uzinduzi wa hii miongozo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu tulipewa maelekezo kuanza mara moja utekelezaji wake, na awali kama taasisi tulikuwa tayari tumeshaanza kuandaa miongozo yetu na sasa tupo katika nafasi nzuri ya utekelezaji kwa kuwa inakwenda sambamba,” amesema Bw. Saiteru

Hatahivyo, amesema hatua inayofuata ni kuandaa nyaraka ya upimaji utayari wa taasisi wa kufanya kazi ya ufuatiliaji na tathmini.

Mwakilishi wa washiriki, Mhandisi Cecilia Kalangi ameshukuru kwa taasisi kuendesha mafunzo haya, ambayo yatasaidia kupata ufumbuzi wa haraka kwenye miradi yenye changamoto tangu awali.

Nawe Mha. Magesa Chacha, Mkuu wa Idara ya Mipango kutoka TANROADS mkoa wa Mwanza amesema washiriki wameweza kujifunza namna ya kufanya ufuatilia na tathmini kwa kuzingatia maono ya Dunia na ya serikali ya mwaka 2025 na pia mifumo iliyoibuliwa na Wizara ya Ujenzi ya kuweka taarifa zote za miradi.

“Nawasihi washiriki wenzangu kuzingatia kila hatua ya mafunzo haya kwani ndio mwarubaini ya miradi ambayo baada ya kuanza inaonekana ikiwa na changamoto, wakati ingeweza kutambulika katika hatua za awali ingetatuliwa mapema,” amesisitiza Mha. Kalangi.

Naye mwezeshaji Bw. Chalton Meena kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu amesema ofisi hiyo inasimamia utendaji wa serikali kwenye wizara na taasisi zake, hivyo wote hawana budi kufuata mwongozo huo wa mwaka 2024.

Bw. Meena amezitaja nyaraka hizo kuwa ni Mwongozo wa Tathmini wa Kitaifa (National Evaluation Manual); Mwongozo wa Usimamizi wa Tathmini nchini na Ufuatiliaji na Tathimini (Monitoring & Evaluation Readness Assessment Tool for Government Institutions).

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa