Masoud Masasi,Dodoma
WIZARA ya Nishati na Madini imesema iko katika hatua za mwisho
kukamilisha maandalizi ya sera,sheria na mpango kabambe wa matumizi ya
gesi asili hapa nchini ambapo itaweza kusaidia kuondokana na matumizi
ya nishati ya mkaa pamoja na tatizo la umeme.
Hayo yalibainishwa jana mjini Dodoma na Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari juu ya ugunduzi wa gesi na mafuta asili hapa nchini.
Muhongo alisema mchakato huo unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi
Septemba mwaka huu kabla ya kuwasilishwa rasmi serikalini kwa ajili
ya kupitishwa ambapo amesema marekebisho madogo kwenye sheria ya gesi
na mpango wa matumizi ya gesi yanaendelea kufanyika sambamba na sera
ya gesi.
“Tuko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya sera,sheria na
mpango kabambe wa matumizi ya gesi asili nchini na baada ya miaka
kadhaa tutaondokana na matumizi ya nishati ya mkaa na kuni majumbani
na kuanza kutumia gesi ambapo ifikapo mwezi julai mwaka huu rasimu ya
kwanza itakuwa tayari”alisema Muhongo.
Akizungumzia mchakato wa ugunduzi wa gesi asili nchini,Waziri Muhongo
alisema kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji wa mafuta na gesi ambapo
amesema kiasi cha gesi asili kilichogundulika katika kina cha maji
marefu kinafikia futi za ujazo 20.97 trilioni katika bahari ya Hindi.
Alisema gesi hiyo inajumuisha kisima Lavan kilichogunduliwa mapema
wiki hii na kampuni ya Statoil kwa kushirikiana kampuni ya Exxon Mobil
ambapo amesema kisima hicho kipo katika kitalu namba mbili Mashariki
mwa Mkoa wa lindi kilometa 80 kutoka nchi kavu.
“Katika kipindi hiki cha miaka mitatu tumekuwa na kasi kubwa ya
utafutaji wa mafuta na gesi asili hapa nchini na tumeweza kugundua
kiasi cha gesi asili katika kina cha maji marefu takribani futi zenye
ujazo wa 20.97 trilioni ikijumuishwa kisima kilichogunduliwa wiki hii
cha lavani mashariki mwa mkoa wa Lindi”alisema.
Alibainisha kuwa makampuni 19 makubwa duniani ya utafutaji wa mafuta
na gesi yapo hapa nchini yapo kwa ajili ya kufanya utafiti ambapo
wameweza kutoa leseni 28 kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo.
Waziri huyo alisema serikali itaendelea kutoa msukumo zaidi kwa
makampuni ya utafutaji mafuta na gesi asili ili yaendelee kufanya
utafiti pamoja na ugunduzi zaidi ambapo amesema itasaidia kuleta
maendeleo ya nchi.
0 comments:
Post a Comment