na Edson Kamukara, Dodoma
SERIKALI imetakiwa kuchukua hatua kuimarisha ulinzi kwenye mitambo ya kuzalisha umeme kutokana na kuwepo kwa tishio la mafisadi kutaka kuihujumu mitambo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Tahadhari hiyo ilitolewa jana bungeni mjini hapa na wabunge Kangi Lugora wa Mwibara (CCM) aliyeungwa mkono na Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) katika mwongozo wao kwa Spika wakitaka vyombo vya ulinzi kulinda mitambo hiyo.
“Mheshimiwa Naibu Spika juzi hapa wakati Waziri wa Nishati na Madini akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara yake, alitueleza kuwa mgawo wa umeme hautakuwepo tena, sijui kama anaweza kutuhakikishia ni tahadhari gani amechukua,” alihoji.
Lugora aliongeza kuwa mitambo ya kuzalisha umeme yote inamilikiwa na makampuni binafsi ambayo hayana ulinzi imara, kwamba kutokana na mafisadi wa makampuni ya mafuta kushindwa kupenyeza ajenda yao TANESCO, wameanza njama za kutaka kuihujumu mitambo hiyo ili kutaka kudhihirisha uongo wao kuwa nchi ina matatizo ya umeme.
Hivyo aliomba mwongozo wa Spika kama serikali ina taarifa hizo na imechukua hatua gani, hoja ambayo iliungwa mkono na Mbatia akisema kuwa vyombo vya dola kama Jeshi la Wananchi vinapaswa kulinda mitambo hiyo.
“Mafisadi hawa wanafanya kila mbinu kutaka kuhakikisha wanaidhoofisha TANESCO, sasa naomba mwongozo wako Mheshimiwa Naibu Spika wa ni kwanini JWTZ au JKT au Jeshi la Polisi wasipewe kazi ya kulinda mitambo yetu kwenye vyanzo vyote na maeneo yote zinapopita nyaya zenye msongo mkubwa,” alisema.
Mbatia alisema ufisadi ni mfumo, kwani vita hiyo iko ndani na nje ya TANESCO na hivyo kuitahadharisha serikali kutopuuza vitisho vya hujuma hizo za mitambo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment