Masoud Masasi, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi ameshauri waendesha pikipiki (bodaboda) kupimwa akili kwanza kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo madereva wa abiria, mizigo na pikipiki mjini Dodoma juzi, Nchimbi alisema madereva hao huendesha pikipiki zao kama watu waliorukwa na akili.
Alisema madereva hao wa pikikipiki wamekuwa wakiendesha kwa mwendo wa kasi bila ya kufuata sheria za barabarani jambo linalofanya kutokea kwa ajali za mara kwa mara.
Nchimbi alisema sasa iko haja kwa madereva hao kupelekwa Hospitali ya Mirembe ili kupimwa akili kutokana na yeye kuhisi wana matatizo hayo kutokana na uendeshaji mbovu wa pikipiki hizo.
“Ukiwaona wanavyoendesha pikipiki hizi jamani lazima utahisi tu hawa jamaa wanatakiwa kupelekwa Mirembe kupimwa akili kwa kuwa wakati mwingine inawezekana ni matatizo tu ya akili inabidi wapelekwe Mirembe,” alisema Nchimbi .
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani hapa kuwakamata madereva wa bodaboda na taksi watakaokuwa wakiendesha kwa fujo vyombo hivyo katika kipindi cha Maonyesho ya Nane Nane kwa madai ya kuwahi abiria.
“Kuna tabia ya hawa madereva wa pikipiki na taksi wamekuwa wakiendesha kwa kasi katika kipindi cha Maonyesho ya Nane Nane, Polisi wakamateni, wapokonyeni leseni na msiwaruhusu mpaka maonyesho yaishe kwa sababu wanaweza kusababisha ajali hawa,” alisema.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo, mgeni rasmi Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba alisema ajali za pikipiki zimekuwa nyingi kutokana na madereva wake kutofuata sheria za barabarani na kusema hili litawamaliza.
“Hospitali nyingi katika mkoa wa Mwanza na Dar es Salaam wodi zake zina majina ya Sanlg, Better na nyinginezo na hii inatokana na ajali za mara kwa mara za pikipiki jambo lililofanya kuitwa majina hayo ambayo si vizuri,” alisema Naibu waziri huyo.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment