Masoud Masasi- Dodoma yetu Blog
IMEELEZWA kuwa elimu inayotolewa na asasi za kiraia kuhusiana na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika halmashauri nchini imeanza kuzaa matunda kwa wananchi kuhoji matumizi ya fedha hizo.
Hayo yameelezwa na mratibu wa mtandao wa asasi za kiraia mkoani Dodoma (Ngonedo) Edward Mbogo wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ufafiti wa ufatiliaji wa mradi wa PETS kwa wadau na waandishi wa habari mkoani Dodoma.
Mbogo amesema kuwa elimu inayotolewa na asasi za kiraia kuhusiana na umuhimu wa wananchi kuhoji matumizi ya fedha za umma zinazopelekwa kwenye halmashauri imeanza kuzaa matunda kwa kuwa sasa wananchi wanaelewa umuhimu wa kujua matumizi ya kila shilingi inavyotumika.
Amesema kumekuwepo na muwamko kwa wananchi kuhoji fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri zao na jinsi zinavyotumika tofauti na zamani ambapo wananchi walikuwa na woga wa kuhoji fedha hizo kwa kuwa hawakuwa na elimu na wala walikuwa hawajui kama kuna fedha zinazoingia kwenye halmashauri kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.
Afafanua kuwa kutokana na elimu hiyo wananchi wa mkoa wa Dodoma hivi sasa hawahitaji kushirikishwa katika miradi inayoanzishwa katika halmashauri zao bali wanashiriki wao wenyewe bila kusubiri kushirikishwa miradi hiyo kuanzia kwenye bajeti ya miradi husika
Amesema lengo la asasi za kiraia kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha wananchi kupata uelewa wa miradi mbali mbali inayowahusu wananchi na ambayo fedha zake zinapitia halmashauri, kwa kujua fedha zilizotumwa na thamani ya miradi iliyoanzishwa kama inaendana na thamani ya fedha.
Ameongeza kusema kuwa mradi huo wa kutoa elimu kuhusiana na matumizi ya fedha za umma umefadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil society ambapo ulianza mwaka 2009 hadi mwaka huu ambapo zaidi ya shilingi milioni 190 zilitumika kwa ajili ya kutoa elimu hiyo kwa wilaya zote sita za mkoa wa Dodoma.
Amezitaja wilaya hizo kuwa ni pamoja na wilaya ya Dodoma Mjini, Kondoa, Chamwino, Bahi, Kongwa na wilaya ya Mpwapwa ambapo wilaya ya Chemba haikupata elimu hiyo kwa kuwa ilikuwa bado haijaanzishwa.
0 comments:
Post a Comment