Home » » LUSINDE AIMWAGIA SIFA CHADEMA

LUSINDE AIMWAGIA SIFA CHADEMA

na Danson Kaijage, Dodoma
MGULI wa siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kiongozi aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, Balozi Job Lusinde, amesema CHADEMA ni miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani ambavyo vinafanya vizuri katika kukuza chama na kutangaza sera zake.
Balozi Lusinde alitoa kauli hiyo katika mahojiano na Tanzania Daima, akisema kuwa chama hicho kimeweza kutumia nafasi mbalimbali kutangaza sera zake kwa kutumia maandamano ya nchi nzima.
Alisema kutokana na hali hiyo, mwaka 2015 hautakuwa mwepesi kwa CCM, hivyo kinapaswa kujipanga zaidi ili kufanikisha matarajio yao.
“Sitegemei uchaguzi wa mwaka 2015 kama utakuwa mwepesi, bali kinachotakiwa kwa CCM ni kujipanga, maana kila mwaka uchaguzi unakuwa na changamoto zake. Uchaguzi uliopita ulikuwa mgumu na unaokuja utakuwa mgumu zaidi,” alisema Balozi Lusinde.
Akizungumzia suala ya wana CCM kufikia hatua ya kutishiana silaha, alisema ni aibu kwa chama kikubwa kama hicho kuonesha hali hiyo.
Alisema kwa kawaida matukio ya kupishana na kutokuelewana yanatokea katika kila chama hususan kipindi cha chaguzi, lakini uchaguzi unapomalizika makundi huvunjwa na kuanza kufanya kazi kwa mshikamano.
“Hata wakati wa chama kimoja, wakati wa chaguzi kulikuwa na matatizo, lakini yalikuwa hayatangazwi katika vyombo vya habari, bali mambo hayo yalikuwa yakiishia katika vikao mbalimbali na kuyatolea maamuzi ambayo yanaleta ufumbuzi,” alisema
Chanzo: Tanzania Daima

1 comments:

Anonymous said...

Hongera sana mzee kwa kuona hilo. Nchi yetu kwasasa ina tawaliwa na vibaka mafisadi wanafiki n.k kwa nia ya kuchukua kila kitu kwa manufaa ya familia zao. Naamini watanzania wengi wameamua kuachana na chama cha majambazi 'ccm' na kuhamia cdm chenye matumaini.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa