na Danson Kaijage, Dodoma
MAMA mjamzito,
Sarah Malima (17), mkazi wa Michese, amenusurika kufa na baada ya kujifungulia
chini ya sakafu wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kutokana na manesi
kushindwa kumhudumia huku wakimtupia maneno ya kejeli.
Tukio hilo
lilitokea hospitalini hapo jana baada ya mama huyo kuwataka manesi waliokuwapo
kumsaidia baada ya kuzidiwa na uchungu.
Sarah alisema
kabla ya kujifungulia wodini, aliwaomba manesi kumpeleka chumba cha
kujifungulia, lakini hawakumsikiliza na badala yake waliendelea kula chips huku
wakimtolea maneno ya kebehi.
Tanzania Daima
ilishuhudia tukio hilo ambalo liliwasikitisha watu waliokuwa hospitali hapo na
mama huyo alisema kuanzia saa 10:30 jioni aliwaambia manesi wamsaidie, lakini
hawakumsikiliza.
“Nilianza
kuwaelezea muda mrefu manesi wanisaidie, kwani nilikuwa nasikia uchungu, lakini
nilikuwa nikijibiwa majibu ya ovyo na baadaye waliniambia nisiwashobokee kwani
wanakula.
“Niliendelea
kujisikia vibaya hadi kufikia hatua ya kujifungulia sakafuni, jambo ambalo ni
hatari, lakini namshukuru Mungu kwani nimenusurika kufa kutokana na uzembe wa
manesi hawa,” alisema.
Kwa upande wao
manesi waliohusika na tukio hilo hawakutaka kuzungumza jambo lolote
walipoulizwa kwa madai kuwa wao si wasemaji.
Naye Kaimu
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Nassoro Mzee, alipoulizwa alisema kuwa hilo
ni tatizo dogo inashangaza kuona watu wanalilalamikia.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment