Home » » OFISA AFYA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU

OFISA AFYA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU

Na Debora Sanja, Dodoma
OFISA Afya wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Gombo Dotto, amefikishwa mahakamani jana kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 3.2. Ofisa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hassan Momba.
Akimsomea mashitaka yake, Mwanasheria wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Emmanuel Meta, alisema ofisa huyo anakabiliwa na makosa 11 ambayo yote ni ya ubadhirifu wa fedha.

Alisema mshitakiwa huyo pamoja na mwenzake wanatuhumiwa kugushi hati ya malipo yenye thamani ya Sh milioni 3.2 kwa lengo la kumuibia mwajiri wake.

Alisema Mei 28, 2009, mshitakiwa huyo akishirikiana na mhudumu wa Mgahawa wa 4F, Hassan Duma, kugushi hati ya malipo namba 365 kwa nia ya kumuibia muajiri wake Sh 900,000.

Alisema kwa mujibu wa maelezo ya mtuhumiwa, alidai fedha hizo zilitumika kwa viburudisho kwa vituo vya afya vinne jambo ambalo si kweli.

“Katika shitaka jingine mtuhumiwa anatuhumiwa kugushi hati ya malipo ambayo ilionyesha vituo sita vya afya vimepewa Sh 50,000 kama fedha kwa ajili ya muda wa maongezi,” alisema Meta.

Hakimu aliwahoji washitakiwa hao na wote walikana mashitaka yao na wapo nje kwa dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 11, mwaka huu na upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa