Home » » SERIKALI YAOMBWA KUKARABATI BWAWA LA IKOWA

SERIKALI YAOMBWA KUKARABATI BWAWA LA IKOWA

Na Debora Sanja, Dodoma
MBUNGE wa Chilonwa (CCM), Hezekiah Chibulunje, ameiomba Serikali kukarabati Bwawa la Ikowa, ambalo ni chanzo cha maji katika Skimu ya Umwagiliaji iliyoko katika Kijiji cha Chalinze, jimboni humo.

Akizungumza na MTANZANIA katika eneo la bwawa hilo, alisema viongozi wengi wamekuwa wakienda kuangalia skimu hiyo na eneo linalolimwa kwa umwagiliaji, lakini hawafiki kuona chanzo cha maji.

Alisema ni vizuri viongozi mbalimbali kufika katika chanzo cha maji cha skimu hiyo ambacho ni Bwawa la Ikowa kwa ajili kuona changamoto zinazolikabili bwawa hilo, ikiwamo uharibifu wa mazingira.

“Viongozi wengi wanakwenda kuangalia mafanikio ya kilimo cha umwagiliaji Chalinze, lakini wanaishia katika mashamba ya wananchi bila kufika katika chanzo cha mafanikio, ambacho ni Bwawa la Ikowa.

“Bwawa hilo lilijengwa mwaka 1957 kwa madhumuni ya kuwapatia wananchi maji ya umwagiliaji mashamba, eneo la kunyweshea mifugo na uvuvi.

“Hata hivyo Skimu ya Umwagiliaji iliyojengwa kutokea katika bwawa hilo ilififia miaka 72 na kufufuliwa mwaka 2001 na kuendelea kukarabatiwa kila mwaka.

“Changamoto kubwa iliyopo ni uharibifu wa mazingira ya bwawa hilo, kwa kuwa wafugaji wanakwenda kunywesha mifugo, hivyo bwawa kushindwa kuhifadhi maji katika kipindi cha mwaka mzima,” alisema Chibulunje.

Aidha, alisema ipo skimu iliyokuwa imejengwa kwa ajili ya kutolea maji na kupeleka sehemu ya kunyweshea mifugo lakini kwa sasa skimu hiyo imeziba na kumekuwapo na nyasi nyingi.

“Malengo yetu ni kufufua sehemu hiyo ili wafugaji wawe na eneo lao, wakulima wawe na lao na wavuvi la kwao bila kuathiri uhai wa bwawa,” alisema.

Alisema fedha zinahitajika kwa ajili ya kukarabati lango la kutolea maji na kuongeza kina cha maji na hatimaye skimu hiyo iwe na chanzo cha maji cha uhakika kwa kipindi cha mwaka mzima

Alisema skimu hiyo ina ekari 96 zinazotumika kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kulima mbogamboga, ikiwamo zao la maharage.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa